Kiungo na Nahodha wa Young Africans Pappy Kabamba Tshishimbi amesema wana matumai ya kuendeleza ubabe dhidi ya Simba SC, kama walivyofanya kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Machi 08.

Simba SC na Young Africans watakutana Julai 12 katika mchezo wa Nusu Fainali Kombe La Shirikisho (ASFC), ikiwa ni mara ya tatu kwa miamba hiyo kukutana mwaka huu.

Mwezi Januari wababe hao walikutana katika mchezo wa mzunguuko wa kwanza Ligi Kuu Tanzania bara, na kutoshana nguvu kwa kufungana mabao mawili kwa mawili, mara ya pili ilikua Machi 08 ambapo Young Africans waliibuka washindi kwa bao moja (Mzunguuko wa pili Ligi Kuu Tanzania Bara).

Tshishimbi ambaye ni raia wa DR Congo amesema anatambua wadau wengi wa soka wanaamini Young Africans ni dhaifu, lakini ukweli ni kwamba wapo vizuri, na ushindi katika mchezo huo utatoa hatma ya kikosi chao kurejea anga za kimataifa msimu ujao.

“Unajua Simba tayari wao wana uhakika wa kucheza mashindano ya kimataifa, watashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa hiyo mchezo huu lengo lao litakuwa moja tu kutokukubali kufungwa mara mbili na sisi (Young Africans),” alisema Tshishimbi ambaye Kocha Luc Eymael amesisitiza kuwa atakuwa fiti kufikia siku ya mchezo huo.

“Tunaitaka tiketi hiyo hata kwa kuvunjika miguu, tunahitaji kushiriki kimataifa na nafasi kubwa na ngumu ni hapa, lazima tuvuke kwa ushindi wowote ndio maana nasema hii ni fainali kwetu.”

Hata hivyo Tshishimbi amesema hawatakubali kufungwa na Simba SC, kwani kama watakubali hali hiyo watakuwa wamemaliza msimu wa 2019/20 bila taji lolote msimu huu.

“Tunatakiwa kulinda heshima ya mashabiki na viongozi wetu, nafasi pekee ya kupata kombe msimu huu ni hapa, Simba kombe wanalo – tena lenye heshima, wachezaji tunalijua hilo na nimewakumbusha wenzangu na tunaendelea kukumbushana,” alisema.

Young Africans walitinga hatua ya Nusu Fainali Kombe La Shirikisho (ASFC) kwa kuifunga Kagera Sugar mabao mawili kwa moja, huku Simba SC wakiibomoa Azam FC mabao mawili kwa sifuri Uwanja wa Taifa, Dar es salaam.

FBI wanavyomnyoosha ‘Hushpuppi’, mwizi nguli mtandaoni
Takukuru yawajibu Chadema kuhusu kuwahoji wabunge 69