Shirika la Mawasiliano Nchini (TTCL) katika kipindi cha siku 30 limeweza kusajili wateja wapya 215,000, ikiwa ni Mpango Mkakati wa Shirika hilo katika kujiinua kibiashara na kuongeza wigo huduma ya Mawasiliano kwa Watanzania ikiwa ni utekezaji wa agizo la Rais Dkt. John Magufuli.

Hayo yamesemwa katika Maonyesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere na Meneja Mawasiliano wa TTCL, Nicodemus Mushi ambapo amesema kuwa Shirika hilo limetekeleza kwa vitendo agizo la Rais Dkt. John Magufuli alilolitoa kwa Shirika hilo tarehe 21 Mei, mwaka huu.

Mushi amesema kuwa hadi sasa huduma za Mawasiliano za Kampuni hiyo katika Mfumo wa 4G zinapatikana katika Mikoa 16 nchini na mpango uliopo ni kuhakikisha kuwa maeneo yaliyobaki yanapata huduma za Shirika kupitia Mpango Mkakati wa Shirika hilo uliojiwekea na hivyo kuweza kuleta ushindani wa huduma ya mawasiliano na makampuni mengine nchini.

“Mwaka uliopita tulijiwekea Mpango Mkakati wetu ambao utahakikisha kuwa tunaweza kuleta ushindani na makampuni mengine na hivi sasa kama unavyoona tumeweza kupata wateja wapya 215,000 na kupitia maonesho hayo tutaweza kuongeza wateja wengi zaidi,”amesema Mushi.

Aidha, ameongeza kuwa kwa sasa Shirika hilo limeweza kupata wateja wengi zaidi wakiwemo watumishi wa serikali, ambapo kwa kutambua umuhimu huo, TTCL imeanzisha kifurushi maalum cha ‘watumishi pack’ ambacho kinaweza kutumiwa na wafanyakazi wote wa serikali kwa kuweza kukamilisha taratibu mbalimbali ikiwemo vitambulisho vya kazi.

Hata hivyo, amesema kuwa malengo ya Taasisi hiyo ni kuweza kujipanga ili kuendelea kutoa huduma bora na zenye viwango ili kuweza kuongoza na kuwa kampuni bora ya mawasiliano inayotoa huduma bora kwa wateja wake nchini.

Video: TFS yaandaa ziara ya utalii hifadhi ya Magamba Lushoto
Wachimbaji wadogo wadogo wa madini wapigwa msasa