Kocha wa Klabu ya Paris Saint-Germain (PSG), Thomas Tuchel amezungumzia uwezekano wa Neymar da Silva Santos Junior kuwa sehemu ya kikosi kitakachoikabili Manchester United mwezi ujao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Tuchel ameeleza kuwa mchezaji huyo ambaye hivi sasa ni majeruhi ana uwezekano mdogo sana wa kuwa sehemu ya kikosi chake dhidi ya Wekundu hao wa Old Trafford, Februari 12 kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.

“Itakuwa vigumu sana. Kama nilivyoelezea ni mapema sana kuzungumzia lini Neymar atarejea uwanjani. Tunapaswa kusubiri wiki ya kwanza, ambayo ni muhimu sana pamoja na jinsi anavyoendelea na matibabu,” alisema Tuchel.

“Ni baada ya hapo tu ndio tunaweza kuwa na uelekeo. Lakini itakuwa vigumu sana, hii sio siri,” alisisitiza.

Mchezaji huyo wa Brazil alipata tena majeraha baada ya kuumia mguu wake wa kulia walipokutana na Strasbourg kwenye Kombe la Ufaransa  wiki iliyopita ambapo walijizolea ushindi wa 2-0.

Jana, PSG waliingia uwanjani bila Neymar lakini walifanikiwa kuwachapa Rennes 4-1, katika mchezo wa Ligue 1, huku Edinson Cavani aking’ara kwa kupachika magoli mawili.

Video: Msigwa amjibu Askofu Kakobe, 'Amekengeuka sana huyu mzee'
Chadema wamgomea Askofu Kakobe, 'katubu mwenyewe'