Meneja wa Mabingwa wa Soka Barani Ulaya Chelsea FC Thomas Tuchel, anaamini Mlinda Lango wa kikosi chake Édouard Osoque Mendy hajaathiriwa na mpango wa kuachwa orodha ya wanaowania Ballon d’Or.

Tuchel ametoa kauli hiyo ya kijasiri, kufuatia Mlinda Lango huyo kutoka nchini Senegal kuonesha kiwango kikubwa kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Brentford, ambapo Chelsea walichomoza na ushindi wa bao 1-0.

Meneja huyo kutoka nchini Ujerumani anaamini Mendy anatakiwa kutambulika kwa kiwango chake na hivyo anahitaji kutunukiwa tuzo yake binafsi, lakini hadhani kama kipa wake huyo atakuwa analifikiria sana hilo.

Alipoulizwa kama Mendy alitakiwa kuwa kwenye orodha hiyo, Tuchel aliwaambia waandishi wa habari: “Ndio, lakini nina furaha na muhimu zaidi ni kiwango chake kuliko hiyo orodha.

“Sidhani kama hilo linamsumbua, natumaini halimkwazi kabisa, kwa sababu hata mimi silifikirii, ninachoangalia ni kiwango chake na anavyoisaidia timu.”

Katika mchezo dhidi ya Brentford, Mendy aliokoa hatari kwa asilimia 91.2 pia aliongoza kati ya Walinda Lango waliocheza angalau michezo sita kwenye msimu wa 2020-21 katika mashindano hayo.

Wakati wachezaji wenzake wa Chelsea, Cesar Azpilicueta, Jorginho, N’Golo Kante na Mason Mount walitajwa kwenye orodha ya wachezaji 30 wanaowania tuzo ya Ballon d’Or, Mendy ameachwa.

Ethiopia yakataa chakula
Fiston Mayele atema cheche Songea