Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus Mwangela ameunda timu ya kuchunguza tuhuma 13 zilizoelekezwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ileje na kuelekeza kuwa timu hiyo ifanye uchunguzi huo kwa haraka.

Amefikia uamuzi huo mara baada ya majadiliano ya kikao cha pamoja na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje waliomuandikia barua wakiwasilisha tuhuma za kutoridhishwa na utendaji wa Mkurugenzi huyo.

“Nimefanya ziara Wilaya ya Ileje baada ya kupata barua kutoka kwa Madiwani wakimtuhumu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ileje, kabla ya kufanya maamuzi tumejadiliana na nimefikia uamuzi wa kuunda tume ambayo itachunguza tuhuma zote 13 walizowasilisha,”amesema Brig. Jen. (Mst) Mwangela.

Amesema kuwa kazi kubwa ya tume hiyo ni kuhakikisha wanapata ukweli na uhalisia juu ya tuhuma hizo huku akielezea kuwa moja ya tuhuma ni udhaifu katika kukusanya mapato.

“Kuna tuhuma ambazo tunaona zina ukweli mfano Ileje haijafanya vyema katika suala la ukusanyaji wa mapato, sasa tumebakiza mwezi mmoja mwaka wa fedha uishe lakini wamefikia asilimia 58 tu ya makusanyo ambapo ni asilimia ndogo ikiwa lengo ni angalau zaidi ya asilimia 80 kwa hiyo hapo kuna dalili za uvujishaji wa mapato”, ameongeza Brig. Jen. (Mst) Mwangela

Aidha, ameongeza kuwa licha ya kwamba uchunguzi unaendelea ametoa maelekezo na mikakati ambayo itasaidia kuhakikisha kazi ya ukusanyaji wa mapato inaendelea vizuri.

Hata hivyo, baadhi ya tuhuma ambazo Madiwani wamezielekeza kwa Mkurugenzi wa halmashauri ni pamoja na matumizi mabaya ya ofisi na tuhuma katika masuala ya nidhamu.

Nchi 21 zashiriki Uchaguzi wa bunge la Ulaya
Mbunge asukumwa ndani baada ya kupingana na mkuu wa mkoa