Waziri wa TAMISEMI, Innocent Bashungwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Apoo Tindwa kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za kusaidia maendeleo kwa jamii (CSR) kutoka mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara.

Apoo ambaye kabla ya kuhamishiwa mkoani Mtwara alikuwa mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Tarime vijijini ambapo pamoja na watu wengine wanatuhumiwa  kwa ubadhirifu wa zaidi ya Sh5.6 bilioni zilizotolewa na mgodi huo kwaajili ya miradi ya maendeleo katika vijiji 11 vinavyozunguka mgodi huo uliopo wilayani Tarime.

Bashungwa amtengaza maamuzi hayo Mei 6, 2022 katika kijiji cha Genkuru wilayani Tarime baada ya kufanya ukaguzi wa ujenzi wa kituo cha afya cha Genkuru kilicho gharimu zaidi ya Sh700 milioni ambacho hadi sasa hakijakamilika licha ya kugharimu kiasi hicho cha fedha, fedha ambazo ni sehemu ya fedha za CSR.

Pamoja na hatua hiyo ameonya kuwa, kiongozi yeyote atakayefanya mchezo na fedha za serikali zinazotolewa kutekeleza miradi kwa Wananchi atachukuliwa hatua kali zaidi bila kufumbiwa macho

Amesema, serikali haipo tayari kuona fedha inazozitoa kutekeleza miradi ya Wananchi zinatafunwa na kushindwa kuwanufaisha Wananchi hivyo amewataka Watumishi wa Serikali waliopewa dhamana ya uongozi kusimamia vyema fedha zinazotolewa zilete tija kwa wananchi.

Aidha, Waziri Bashungwa ameagiza ifikapo Juni 30, 2022 Kituo cha Afya Cha Genkuru kianze kutoa huduma huku Mkurugenzi wa Afya akitakiwa kutoa fedha za kununua mashine ya x-ray kwa ajili ya kituo hicho.

Aidha, Waziri Bashungwa, amesema dhamira ya Serikali ni kuona fedha zote zinazotolewa zinawanufaisha Wananchi huku akisema Rais Samia nia yake ni kuona Watanzania wanaendelea kuneemeka na kuondokana na changamoto mbalimbali katika maeneo yao.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Hapi, ametoa wiki mbili kwa Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa Mkoa wa Mara (TAKUKURU) ahakikishe wahusika wote waliohusika na ufujaji wa fedha za miradi ya maendeleo ukiwemk ujenzi wa Kituo cha afya cha Genkuru wanafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.

Dkt. Stergomena: Changamoto ndogo za Mipaka haziwezi kuathiri amani ya Tanzania
Dkt. Stergomena: 'Sifurahishwi na Ujinsia kazini'