Tume ya Madini nchini, imeitaka kampuni ya kuzalisha makaa ya mawe ya TANCOAL, kuacha kuupotosha umma juu ya tozo inazodaiwa na badala yake ilipe deni la Dola za Marekani 10,408,798 la kipindi cha Septemba 2011 hadi Juni 2019.

Akizungumza jana Septemba 16 jijini Dodoma, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Prof. Shukrani Manya amesema kampuni hiyo ilidai kulazimishwa kuuza makaa ya mawe kwa wateja wenye leseni za biashara ya madini hali itakayoongeza gharama za makaa ya mawe.

“Taarifa hizi ni za upotoshaji na zilichapishwa na kampuni ya TANCOAL kupitia tovuti ya www.miningreview.com tarehe 3 Septemba mwaka huu na zimesambazwa kwenye mitandao mingine ya kijamii, jambo ambalo sio sahihi,’’ alisema Prof. Manya.

Profesa Manya alifafanua kuwa kampuni ya TANCOAL kupitia taarifa yake ilidai kuwa Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imeanza kuitoza TANCOAL tozo ya mrabaha kwenye gharama za usafirishaji wa makaa ya mawe kutoka mgodini hadi kwa mtumiaji wa mwisho wa ndani na nje ya nchi.

Aidha, Manya amesema TANCOAL imekuwa ikilipa tozo ya mrabaha kwa kuzingatia thamani ya madini yakiwa yadi ya Kitai, bila kujumuisha gharama za usafirishaji kwenda kwa wateja, jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010.

Ameongeza kuwa utaratibu huo wa malipo umekuwa ukifuatwa na kampuni nyingine zote zinazochimba ama kuuza makaa ya mawe isipokuwa TANCOAL licha ya kuelimishwa mara kwa mara juu ya namna ya kukokotoa malipo ya mrabaha kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010.

“Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kifungu cha 87 (6) kinaelekeza namna ya kukokotoa mrabaha kwa kuzingatia thamani ya madini sokoni (kwa mtumiaji wa mwisho) ambayo inajumuisha gharama za usafirishaji hadi kwa mteja yaani Gross Value’’ amesema Prof. Manya.

Prof. Manya amefafanua kuwa Kifungu cha 18 (1) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kinakataza mtu au kampuni yeyote isipokuwa mmiliki halali wa leseni ya madini au mfanyakazi wa wamiliki wa leseni hizo kumiliki, kusafirisha au kuuza madini bila kuwa na kibali cha kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya katikati akizungumza na waandishi wa habari, kulia ni nyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula

Mkutano huo ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Dkt. Venance Mwase, Mkurugenzi wa Huduma za Tume, William Mtinya, Meneja wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Gift Kilimwomeshi, Meneja wa Leseni, Mhandisi Ramadhani Lwamo na Kaimu Meneja wa Utafiti na Sera, Andendekisye Mbije.

Mwinyi Zahera ampa 'shavu' mchezaji Yanga
PSG kuivaa Real Madrid bila Mbappe, Cavani