Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Tume ya Mipango imefanya ziara katika Mradi wa ujenzi wa Barabara za juu (Flyovers) unaoendelea katika makutano ya barabara za Nyerere/Mandela Jijini Dar es salaam na kuelezwa kuwa utekelezaji wake umefikia asilimia 19.2.

Ziara hiyo imefanyikakwa lengo la kuangalia maendeleo ya mradi huo huku Mhandisi wa Kampuni ya Ujenzi ya Summitomo Mitsui ambayo inajenga mradi huo Kiyokazu Tsuji, kueleza maendeleo ya ujenzi kwa wataalam kutoka Tume ya Mipango.

Mhandisi huyo amesema kuwa malengo ya awali yalielekeza kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Novemba 2016, utekelezaji uwe umefikia asilimia 21.2 lakini lengo hilo halikufikiwa kutokana na moja ya mashine kupata hitilafu na kulazimika kuagiza wataalam kutoka nje ya nchi kuja kuifanyia matengenezo.

Hata hivyo Mkandarasi huyo amesema kuwa tayari wamejipanga vizuri katika kuhakikisha wanafidia muda uliopotea wakati mashine hiyo ilipokuwa haifanyi kazi ili ujenzi wa barabara hizo ukamilike ndani ya muda uliopangwa.

Kwa upande wa Wataalamu kutoka Tume ya Mipango wamesema kuwa Serikali na Wananchi kwa ujumla wanatarajia kuwa ujenzi huo utakamilika kwa muda uliopangwa hivyo Mkandarasi huyo ana wajibu wa kufanya kila linalowezekana ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

Ujenzi huo unaotekelezwa kwa miezi 35 kauanzia Disemba 1, 2015 hadi Oktoba 31, 2018 unalenga kupunguza tatizo la msongamano wa magari na kuboresha huduma za usafiri katika Jiji la Dar es Salaam.

Shaka awataka watendaji UVCCM kujitathmini
Joe Biden amtaka Trump kujitambua