Tume ya Mipango imekamilisha zoezi la kuandaa wataalamu wanaotarajiwa kutoa mafunzo juu ya usimamizi na utayarishaji wa miradi ya uwekezaji katika sekta ya umma kwa maofisa wa serikali walio chini ya Idara za Sera na Mipango na zile za Uwekezaji katika Wizara, Mikoa, Halmashauri, Mashirika pamoja na Taasisi mabalimbali za Umma hapa nchini.

Akifunga mafunzo hayo mwishoni mwa juma, Naibu Katibu Mtendaji kutoka Tume ya Mipango anayesimamia Klasta ya Biashara za Kimataifa na Mahusiano ya Uchumi, Bw. Paul Sangawe alisema kuwa katika awamu hii ambapo Shilingi trilioni 59 kati ya trilioni 107 zinatarajiwa kutolewa na Serikali pekee katika kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, Serikali imeamua kujipanga upya ili kuhakikisha miradi yote itakayoanzishwa inaleta tija kwa wananchi.

“Tumeamua kujiandaa mapema kwa sababu tunatarajia miradi mingi mikubwa itaanzishwa katika kipindi hiki cha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP II). Hivyo, ni muhimu huko mtakapoelekea kutoa mafunzo mhakikishe mnatoa mbinu sahihi za kukabili changamoto zinazojitokeza katika kutayarisha, kutekeleza na kusimamia miradi ya maendeleo”, Alisema Bw. Sangawe.

Sangawe aliongeza  kuwa baada ya mafunzo hayo kuwafikia walengwa wote hakutakuwa na sababu kwa maofisa wa serikali kushindwa kuandaa, kutekeleza, kusimamia au kutoa ushauri sahihi pale serikali inapofanya uwekezaji kwa ajili ya  miradi ya maendeleo.

Akitoa neno la shukrani kwa uongozi wa Tume ya Mipango kwa niaba ya wahitimu wote, Mchumi Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bi. Sauda Ponda alisema kuwa wahitimu wote walipata fursa ya kujadili, kuuliza na kufanya mazoezi mbalimbali katika vikundi kwa lengo la kuongeza uelewa na kuimarisha uwezo  kwa ajili ya kwenda kutoa mafunzo kwa wahusika.

“Kwa niaba ya wenzangu wote napenda kutoa shukrani za pekee kwa Tume ya Mipango kwa kuandaa mafunzo haya, waalimu wetu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wametufundisha vizuri na wametupa mazoezi ya kutosha na sote tuko tayari kwenda kutoa elimu hii kwa wenzetu,”. Alisema Bi. Ponda.

Wataalamu hao waliotumia siku tano kuchambua kwa kina Mwongozo wa Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi ya Uwekezaji katika sekta ya Umma ambao ndio unaopaswa kufuatwa katika kutekeleza miradi yote ya serikali, wanatarajiwa kugawanyika katika makundi mbalimbali yatakayotoa mafunzo kikanda ambapo zoezi hilo litaanza  tarehe 22 mwezi huu

Ndege Ndefu Kuliko Zote Duniani Yapaa Uingereza
Ndanda FC Washindwa Kufurukuta, Wakubali Kufungwa 3-1