Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Prof. Ibrahim Lipumba amempongeza Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma kwa kuboresha huduma mbalimbali za mahakama.

Ameyasema jijini Dar es salaam wakati wa kilele cha wiki ya sheria, ambapo amesema kuwa kwasasa huduma za mahakama zimeboreshwa kiasi cha kupunguza malalamiko yaliyokuwa yakitolewa  na wananchi hapo awali.

Amesema kuwa kitendo cha mahakama kuzindua mahakama inayotembea ni kitendo cha kupongezwa kwani ni moja ya hatua kubwa iliyofanywa na mahakama hivyo itawarahisishia wananchi kuweza kupata huduma popote walipo.

”Nampongeza sana Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma kwa kuweza kuisimamia vizuri mahakama na kuweza kuboresha huduma zake, hasa kwenye hili la kuzindua mahakama inayotembea, kwasababu itaweza kurahisisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi,”amesema Prof. Lipumba

Aidha, Prof. Lipumba amemtaka Jaji huyo kuendelea kufanyia marekebisho kasoro mbalimbali ambazo zmekuwa zikilalamikiwa na wadau mbalimbali wa sheria ili kuweza kuboresha zaidi utoaji wa huduma.

Hata hivyo, kilele cha wiki ya sheria kilihitimishwa jijini Dar es salaam na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.

DC Kabeho azitaka mahakama wilayani Tarime kutenda haki
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Februari 7, 2019