Mbunge wa Singida Mashariki ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amepinga agizo lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli linalowataka wabunge na madiwani kufanya mikutano katika maeneo waliochaguliwa bila kuvuka mipaka.

Akizungumza jana muda mfupi baada ya kutoka katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana jijini Dar es Salaam,  kusikiliza kesi ya uchochezi dhidi yake, Lissu alisema kuwa kwa mujibu wa sheria za nchi, Rais hahusiki na uamuzi wa kufanyika mikutano ya hadhara ya kisiasa bali hilo ni jukumu la Mkuu wa Polisi wa Wilaya husika.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Katiba ya nchi hii na sheria zake zote, hana mamlaka yoyote ya kusema lolote au kufanya lolote kuhusiana na mkutano ya hadhara. Mtu anayetambuliwa na sheria kuhusiana na mikuano ni OCD peke yake,” alisema.

Alisema kuwa Sheria inaviruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara mahala popote ndani ya nchi na kwamba Rais alitoa agizo hilo bila kusoma sheria.

Mwanasiasa huyo alisema kuwa kuwaruhusu walioshinda pekee kufanya mikutano, kutavinyima haki vyama vya siasa ambavyo havikufanikiwa kupata ushindi hata katika jimbo moja kama UDP na TLP, hivyo kuvinyima haki ya kufanya siasa.

Aidha, Lissu alisisitiza msimamo wa Chadema kuwa watafanya mikutano na maandamano nchi nzima kuanzia Septemba Mosi kama walivyopanga kwani ni haki yao kikatiba.

“Kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa, vyama vya siasa vina haki ya kufanya maandamano na mikutano ya hadhara,” ananukuliwa.

Alisema kuwa vyama vya upinzani vina haki kama ilivyo kwa chama cha tawala (CCM) na viongozi wake.

Madaktari wasahau taulo ndani ya tumbo la Mgonjwa baada ya upasuaji
Polisi wamtega Msigwa, wamruhusu kufanya mkutano hadi ‘Septemba Mosi’