Uongozi wa Simba SC umeweka wazi kuwa tuzo ambazo wamekomba wachezaji wake kwenye mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kumewaongezea hali ya kujiamini.

Chini ya Kocha Mkuu, Roberto Oliveira Raia wa Brazil usiku wa kuamkia leo Jumamosi (April Mosi), Simba SC ilimaliza kete yake ya mwisho dhidi ya Raja Casablanca mchezo wa hatua ya Makundi huku timu zote zikiwa zimetinga hatua ya Robo Fainali.

Ni Clatous Chama ana tuzo mbili kabatini ikiwa ni ile ya mchezaji bora mechi ya nne pia ana tuzo ya bao bora alilofunga wakati ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Simba 7-0 Horoya, ambapo kwenye mchezo huo alifunga Hat Trick.

Nyota huyo alitajwa kwenye kikosi bora mchezo wanne pamoja na beki Shomari Kapombe kwenye mchezo wa tano alipenya pia kikosi bora akiungana na Jean Baleke, Sadio Kanoute na Kapombe.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alisema kuwa tuzo hizo zinaonyesha ukomavu wa wachezaji wa Simba pamoja na jitihada wanazofanya.

“Kupata tuzo kwa wachezaji wetu na kuwa kwenye kikosi bora hii ni fahari kwetu na inaongeza thamani ya wachezaji pamoja na ukubwa wa timu, pongezi wanastahili na hili linaongeza hali ya kujiamini kwa mechi zetu zote za mashindano ambazo tunacheza.”

“Katika hatua ambayo tunakwenda ya robo fainali inaonyesha kuwa ugumu unazidi kuongezeka huku wachezaji wakizidi kuimarika, tunaamini tutafanya vizuri kwenye haya mashindano makubwa kwa kuwa tuna wachezaji imara,” amesema Ally

Wagonjwa zaidi ya 400 wapatiwa matibabu ya kibingwa
Sally Bolo amuombea msamaha Joash Onyango