Bondia Twaha Kiduku amesema yupo tayari kwa Pambano lake la Kimataifa dhidi ya Bondia kutoka chini Misri Abdo Khared litakalofanyika Jumamosi (Septemba 24), katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mkoani Mtwara.

Kiduku ametoa kauli ya utayari wa Pambano hilo, baada ya kuwasili Mtwara jana Jumatano (Septemba 21), na kupokewa na Mashabiki wake waliojitokeza Uwanja wa Ndege Mkoani humo, huku wengine wakimlaki katika mitaa aliyopita.

Bondia huyo kutoka Mkoani Morogoro amesema amejiandaa vizuri kumkabili Abdo Khared, na ana matumaini mkubwa ya kuwafurahisha watanzania katika pambano hilo la Kimataifa ambalo litapigwa kwa mara ya kwanza mkoani Mtwara.

“Nipo tayari kwa asilimia 99 kumkabili mpinzani wangu, ninajua mpambano utakua na upinzani mkali sana, lakini kwa maandalizi nilioyafanya nina uhakika mambo yatakua mazuri na watanzania watafurahi siku ya Jumamosi,”

“Kilichobaki kwa sasa ni kukaa chini na Makocha wangu ili wanitengeneze kisaikolojia katika siku hizi chache zilizosalia kuelekea pambano langu.” amesema Kiduku

Kuhusu Pambano lake kupigwa Mkoani Mtwara, Twaha Kiduku amesema imekua furaha kwake, kwa sababu hakuwahi kufika mkoani humo na sasa amefika kwa lengo la kuiwakilisha nchi.

Amesema anaamini kufika kwake Mkoani hapo kutamuongezea mashabiki, pia kutamfanya awe na ari kubwa na tofauti na mapambano mengine kwa sababu hatotaka kuwaangusha mashabiki waliojitokeza kumpokea na watakaofuatilia pambano lake kwa njia wa Televisheni Jumamosi (Septemba 24).

“Hii ni mara yangu ya kwanza kufika Mkoani Mtwara, ninaamini ujio wangu hapa umeniongezea mashabiki ambao watakua na mimi bega kwa bega katika Pambano langu, ninawaahidi sitawaangusha.” amesema

Waziri Mchengerwa aampa maagizo mazito Ally Mayay
Habari kuu kwenye magazeti ya leo Septemba 22, 2022