Siku chache baada Bingwa wa masumbwi ya uzito wa juu, Tyson Fury kudai kuwa anaamini Bingwa ambaye hajawahi kupoteza, Anthony Joshua hataweza kukubali kupigana naye ingawa watu wanataka iwe hivyo, timu ya Joshua imebadili upepo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Promota wa A. Joshua, Eddie Hearn amesema kuwa timu yake imeamua kumpa nafasi Tyson Fury kupanda ulingoni na bondia huyo Aprili 13 mwaka huu.

Timu ya Joshua imelipia tayari uwanja wa Wembley kwa ajili ya pambano la Aprili 13 ingawa bado hawajapata uthibitisho wa bondia watakayepambana naye.

Awali, Joshua alipanga kupigana na Deontay Wilder lakini hivi sasa bondia huyo ameeleza kuwa anajikita katika pambano lake la marudiano na Fury.

“Nadhani kwa sasa hivi, kuna nafasi zaidi ya kupigana na Tyson Fury,” amesema Eddie Hearn.

“Ni mtu ambaye anajua kabisa kwamba anaweza kupata pambano hili, kama akilihitaji. Nimeshazungumza naye. Anajua kama anataka kupigana na Joshua, inawezekana kufanyika Aprili 13,” ameongeza.

Hata hivyo, tangazo hilo bado linaleta utata endapo Fury atakuwa anahitaji kumalizana na Wilder kwa pambano la marudiano kufuatia sare yenye utata katika pambano lao la kwanza.

Zikiwa zimebaki miezi mitatu tu kwa pambano la Aprili 13 huku Fury, Wilder na Dillian Whyte ndio ambao wanaotajwa kuwa kwenye nafasi ya kupanda ulingoni dhidi ya A.J mbele ya mashabiki 70,000 kwenye uwanja wa Wembley nchini Uingereza.

Mlango wa kumtaja mmoja kati yao utafungwa ndani ya kipindi cha siku kumi zijazo.

Nairobi: Serikali ya Kenya yaeleza magaidi walivyodhibitiwa
Nairobi: Polisi aliyepoteza bastola bar atiwa mbaroni