Waamuzi watakuwa na mamlaka ya kusimamisha mchezo, endapo mashabiki wa soka wataonyesha vitendo vya ubaguzi wa rangi dhidi ya wachezaji, wakati wa fainali za kombe la mabara ambazo zitaanza mwishoni mwa juma hili nchini Urusi.

Shirikisho la soka duniani FIFA, limepitisha kanuni hiyo, ikiwa ni sehemu ya kupunguza vitendo vya ubaguzi wa rangi ambavyo mara kadhaa huwakuta wachezaji wenye asili ya bara la Afrika.

Urusi imekua na mashabiki watukutu ambao wamejikita katika misingi ya ubaguzi wa rangi, hali ambayo imetoa msukumo kwa FIFA kufikiria kwa kina na kuamua kupitisha kanuni hiyo.

Rais wa FIFA Gianni Infantino amethibitisha kupitishwa kwa kanuni hiyo kwa kusema, dhamira yao ni kuhakikisha mchezo wa soka unakua na usawa kwa lengo la kutokomeza vitendo vya kibaguzi.

Pia kanuni hiyo itatumika katika fainali za kombe la dunia za mwaka 2018, ambapo Urusi wataendelea kuwa wenyeji.

Katika fainali za kombe la mabara mwaka huu, Afrika itawakilishwa na timu ya taifa ya Camaroon(mabingwa wa AFCON wa fainali za mwaka huu zilizounguruma nchini Gabon).

Cameroon imepangwa kundi B, sambamba na mabingwa wa ukanda wa kusini mwa Amerika (Chile), mabingwa wa Asia (Australia) pamoja na mabingwa wa kombe la dunia (Ujerumani).

Kundi A linawajumuisha wenyeji wa fainali hizo (Urusi), mabingwa wa Amerika ya kati na kaskazini (Mexico), mabingwa wa barani Ulaya (Ureno) na mabingwa Oceania (New Zealand).

Simba Waendeleza Furaha Msimbazi
Video Mpya: Biznea feat. Shaa – Mali ya Mungu