Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC), imesema Uchaguzi wa Wabunge katika majimbo ya Muhambwe na Buhigwe mkoani Kigoma pamoja na Uchaguzi wa Madiwani kwenye Kata 18 za Tanzania Bara utafanyika Mei 16, 2021.

Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Dkt. Wilson Mahera, amesema awali Uchaguzi wa Jimbo la Muhambwe ulipangwa kufanyika Mei 2 lakini muda umebadilika kutokana na Jimbo la Buhigwe nalo kuwa wazi, hivyo kuamua Uchaguzi ufanyike siku moja.

Aidha, Dkt Mahera amesema kampeni katika Jimbo la Muhambwe zimesitishwa na zitaanza tena Mei Mosi hadi Mei 15 kama itakavyofanyika Buhigwe.

Jimbo la Muhambwe lipo wazi baada ya aliyekuwa Mbunge wake, Atashasta Nditiye kufariki Dunia, na Jimbo la Buhigwe lipo wazi baada ya Dkt. Philip Mpango aliyekuwa Mbunge kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.

Rais Samia apokea ujumbe wa Kenyatta, aalikwa rasmi
Mkurugenzi Bodi ya Utalii asimamishwa kazi