Mgombea mwenza wa urais wa Azimio La Umoja, Martha Wangari Karua amepiga kura yake katika Shule ya Upili ya Mugumu, eneo bunge la Gichugu, kaunti ya Kirinyaga baada ya kubadilishiwa kituo.

“Nilielekezwa kituo kingine ambapo jina langu lilipatikana. Nimepiga kura na unaweza kuona wino. Tafadhali toka nje na upige kura. Ni siku yetu ya leo kuamua mwelekeo wa nchi hii,” alisema Karua.

Karua alifika katika kituo hicho cha kupiga kura zikiwa zimebaki dakika chache kabla ya saa kumi na mbili asubuhi ambayo kisheria ndiyo muda wa vituo vya kupigia kura kufunguliwa.

Mgombea mwenza huyo wa Raila Odinga ametimiza ahadi yake aliposema atawasili kituoni kutekeleza haki yake ya kidemokrasia kabla ya saa kumi na mbili ya asubuhi.

Akizungumza baada ya zoezi hilo, Karua aliwaomba wapiga kura kujitokeza kwa wingi kutekeleza haki zao za kidemokrasia.

Kufikia saa tisa usiku wa kuamkia leo, tayari foleni ndefu zilianza kushuhudiwa kila mmoja akiwa na hamu ya kumchagua kiongozi wake ambapo vituo vya kupiga kura vilifunguliwa rasmi saa kumi na mbili asubuhi kote nchini Kenya huku wakenya wengi wakijitokeza kuwachagua viongozi wao.

Foleni ndefu ya Wakenya katika hatua ya kila mmoja kumchagua kiongozi wake. Picha:Tuko News

Kwa mujibu wa takwimu za IEBC, wapigakura 22,120,458 waliosajiliwa watapiga kura mwaka huu kuwachagua Wabunge 290 wa Bunge la Kitaifa, madiwani 1,450, maseneta 47, magavana na wawakilishi wanawake, pamoja na mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Uchaguzi wa mwaka huu umevutia vyama 63 vya kisiasa, huku wagombea wasiopungua 11,330 wakiwania viti mbalimbali.

Kenya: Hitilafu zasababisha uchaguzi kuahirishwa
Simba Day yampagawisha Cesar Manzoki