Tume ya uchaguzi nchini Malawi imetangaza matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais uliofanyika juzi Mei 21, ambapo kiongozi wa upinzani anaongoza kwa wingi wa idadi ya kura zilizopigwa.

Kiongozi huyo Lazarus Chakwera, wa chama cha upinzani cha Malawi Party MCP amepata kura 533,217 ambayo ni sawa na asilimia 37.65, Rais Mutharika ndiye anayemfuatia kwa kupata kura 524,247 sawa na asilimia 37.1 huku makamu wa rais Saulos Chilima wa United Transformation Movement akiwa na asilimia 20.76 ya kura zote.

Tayari kiongozi wa chama cha zamani zaidi nchini Malawi Lazarus Chakwera amesema kuwa matokeo hayo ya mapema yanampatia uongozi katika uchaguzi huo mkuu na kusisitiza kuwa kuna jaribio la baadhi ya watu wasiojulikana kuingilia matokeo ya uchaguzi yanayo rushwa moja kwa moja katika kituo kikuu cha uchaguzi mjini Blantyre na kuapa kwamba hatokubali uchakachuaji wowote.

Lakini tume ya uchaguzi nchini humo imetoa wito wa kuwepo kwa utulivu ikisisitiza kuwa ndio yenye uwezo wa kutangaza matokeo hayo licha ya kukiri kwamba inakabiliwa na changamoto za kiufundi katika utangazaji wa matokeo ambayo ni kwa mara ya kwanza nchi hiyo kuhesabu kura kwa njia ya kielektroniki

Takribani raia milioni 6.8 wa Malawi walijisajili kushiriki katika uchaguzi wa kumchagua Rais mpya, wabunge na madiwani na zaidi ya wapigakura milioni saba walipiga kura kwenye uchaguzi huo Mei 21.

Ikumbukwe kuwa katika uchaguzi wa mwaka 2014, Chakwera alishindwa dhidi ya Rais Mutharika na akashindwa kupinga uchaguzi huo Mahakamani.

Serikali kufanya marekebisho ya tozo kwa Wafanyabiashara
JPM afanya uteuzi