Viongozi wa Muungano wa Kenya Kwanza nchini Kenya wanaituhumu serikali ya Kenya kwa kuwatatiza wakandarasi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kutatiza matumizi ya sajili ya kieletroniki na upeperushaji wa kielektroniki wa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Naibu Rais William Ruto akizungumza katika mkutano wa kisiasa katika kaunti ya Kilifi siku ya Ijumaa, Julai 22 amesema wakenya wanatakiwa kupiga kura ya kielekroniki ili kulinda kura za Wakenya.

“Huwezi kulazimisha nchi kuwa na uchaguzi wa sajili za karatasi. Tutakuwa na uchaguzi wa kielektroniki kwa kuwa hiyo ndio njia pekee tutakayolinda kura za Wakenya,” Ruto alisema.

Ruto alielezea Imani ya tume hiyo kupeana matokeo ya kuaminika katika kipute chake na mgombea wa Azimio Raila Odinga akisema kuwa tume hiyo haina majukumu ya kutoa taarifa kwa idara yoyote ya serikali kuhusu oparesheni zake.

“IEBC ni tume huru. Haipigi ripoti kwa yeyote. Huwezi kuwalazimisha kufanya mambo unavyotaka. Tutakuwa na uchaguzi huru na wa haki,” Ruto alisema.

Upigaji kura nchini Kenya hufanyika kwa njia ya kutumia karatasi japo utambuaji wa wapiga kura na upeperushaji wa matokeo hufanyika kwa njia ya kielektroniki.

Mgombea wa urais wa muungano wa Azimio One Kenya, Raila Odinga amekuwa akishinikiza matumizi ya sajili ya karatasi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 ingawa swala hilo limepingwa vikali na IEBC pamoja na kambi ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Wakati huo huo Kinara wa ODM Raila Odinga ameendelea kujivutia kamba ya kuaminika kwa kuwaandikia Wakenya barua kuwaeleza kuhusu azma yake ya kuingia Ikulu na kuwataka Wakenya kuunga mkono Azimio la Umoja.

Kwenye barua hiyo iliyochapishwa mtandaoni, alisema muungano wake wa kisiasa na Martha Karua ulipangwa na Mungu ili waweze kuleta mageuzi nchini.

“Mimi na Mgombea mwenza wangu Martha kwa miaka mingi tumedhihirisha kuwa wanamageuzi wanaopigania taifa letu kunawiri pamoja na Wakenya milioni 50. Kukuja kwetu pamoja wakati huu si ajali au bahati, ni mkono wa Bwana,” Raila aliandika kwenye barua yake.

Zikiwa zimesalia chini ya siku 20 uchaguzi mkuu kufanyika nchini Kenya, Wadadisi wa kisiasa wamesema uchaguzi huu utakuwa baina ya Raila na mgombea wa Kenya Kwanza William Ruto.

Mradi 'ishi vizuri' wazaa matunda uraiani
Serikali yakataa vifo, uharibifu mali za raia