Agosti 9, 2022 Kenya itafanya uchaguzi na matokeo yatamtoa Rais ambaye atakabiliana na matarajio ya wengi katika kuwapunguzia makali ya ongezeko la gharama za maisha, na kuondoa mdororo wa shughuli za kiuchumi ulikochangiwa na athari za Uviko-19 na vita vya Urusi na Ukraine.

Hata hivyo, historia inaonesha kuwa chaguzi za Kenya zimekuwa na nyakati za vurugu hasa baada ya uhuru wa nchi hiyo, ambapo lipo doa la watu wengi kuuawa na mamia kuyahama makazi yao kutokana na machafuko ya uchaguzi kuanzia mwaka 2007.

Ujio wa demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya mwaka 1992, ulisababisha ukabila wa siasa, vyama vingi kuungana na wapenda madaraka wenye ukabila, uwepo wa hali ya kisiasa unaobadilika kila mara na miungano ya makabila ambayo huanzishwa na kusambaratika.

MOI yakanusha kukata viungo madereva ‘bodaboda’

Hatua hii, inaendelea kuashiria kuwa hali ya uchaguzi wa leo nchini Kenya bado unaleta wasiwasi kutokana na mwangwi uliopita ingawa kimtazamo hali ni shwari kwa baadhi ya maeneo.

Na hii, inatokana na kukosekana kwa vyama vinavyoegemea kwenye itikadi thabiti ya kisiasa, utumiaji wa vitambulisho vya kikabila huku manung’uniko ya kikabila yakisalia kuwa msingi mkuu wa uhamasishaji wa kisiasa na tishio la vurugu ingawa mara nyingi matokeo hutegemea mzunguko wa uchaguzi.

Maandalizi haya, ya ukingoni ya Taifa la Kenya kujiandaa na uchaguzi huo mkuu, yanaendelea huku kukiwa na mabadiliko ya baadhi ya ishara za mazungumzo ya kisiasa ya kikabila na vichochezi vyake vya msingi.

Mgombea Urais wa Muungano, William Ruto.

Kama ilivyo katika nchi nyingi ulimwenguni, hili limetokana na athari za Uviko-19 zilizosababisha watu kushughulika na masuala ya afya zao sambamba na chagizo la uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine na kufanya uwepo wa ukosefu wa usawa kati ya raia wa Kenya.

Iwapo jambo hili litabaki kama lilivyo ni wazi kuwa hakutakuwa na vurugu ya kisiasa na huenda mienendo mipya ya kisiasa itathibitika kuwa yenye mgawanyiko wa kimitizamo juu ya hatma za matokeo ya uchaguzi tofauto na hapo awali.

Makala hii inatoa muhtasari wa mienendo ya kisiasa ya sasa, na kubainisha vichochezi na mienendo ya migogoro ya zamani na mipya wakati Kenya ikikaribiia kupiga kura ya uchaguzi wa viongozi watakao liongoza Taifa hilo baada ya uchaguzi mkuu.

Mgombea Urais wa Azimio, Raila Odinga.

Machi, 2018 Rais Uhuru Kenyatta na mpinzani wake wa kisiasa na Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga walisalimiana na kupeana mikono, na hii ikaashiria kumalizika kwa uhasama uliopelekea machafuko ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2017.

Hatua hii ilipopngezwa na kuonekana kama alama muhimu katika Mpango wa Kujenga Madaraja (BBI), ambao ulitaka kuweka misingi ya uponyaji wa kitaifa, ikiwa ni pamoja na ahadi za kukomesha dhuluma za kihistoria za uchaguzi na kuunganisha raia wa Kenya.

Mchambuzi wa mambo ya kisiasa wa Kenya anayeishi eneo la Kericho Job Odhiambo anasema hatua hiyo ilikuwa ni muhimu kwa Taifa la nchi hiyo kwakuwa viongozi wanapogawanyika huleta pia utengamano kwa raia ambao hufuata itikadi zao.

Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyatta.

“Lilikuwa ni jambo la busara sana kwa wawili hawa kupeana mikono maana ikigawanyika serikali na watu hugawanyika na wakigawanyika viongozi kadhalika pia wananchi huwafuata kulingana na jinsi walivyowaelewa kimisimamo kwa hiyo hii iliwaleta watu pamoja,” amesema Odhiambo.

Hata hivyo, matokeo ya mchakato wa BBI katika ripoti iliyozinduliwa Oktoba 2020, ilipendekeza kufanyia marekebisho vipengele mbalimbali vya katiba ya Kenya ili kushughulikia masuala ya ushirikishwaji wa kisiasa na ukosefu wa haki katika uchaguzi, ambapo maoni tofauti yalitolewa na Wakenya.

Na kufuatia kuzinduliwa kwa ripoti ya BBI, Kenyatta na Odinga waliitisha mikutano kote nchini ili kueneza waraka huo, ambapo wengi wa wafuasi wao walitaka marekebisho yaliyopendekezwa kupigiwa kura ya maoni.

Wafuasi wa Naibu Rais, William Ruto, wakachukulia mapendekezo ya BBI kama njia ya kumzuia kuwania urais 2022 na kufanya Ruto na washirika wake kukosoa hadharani mchakato wa BBI, wakisema unalenga kupata nyadhifa za viongozi wa sasa nchini Kenya.

Walidai kuwa hatua hiyo itadhoofisha uhuru wa Mahakama, na kuweka kando maeneo yenye wakazi wachache nchini Kenya huku Ruto akisema Wakenya wana wajibu wa kiraia kuhoji ripoti hiyo, kutatua masuala yenye utata, na kuandaa kura ya maoni isiyopingwa.

Baadaye, wafuasi wa Ruto walizindua mpango wa maombi mbalimbali kuhusiana na uhalali wa marekebisho yaliyopendekezwa ambapo mwezi wa Mei mahakama Kuu ya Kenya ilibatilisha azma ya Rais ya kurekebisha katiba.

Mkenya Mathias Barasa anasema Kamati ya Uongozi ya BBI ilikuwa na ufahamu wa kufanya kazi ndani ya muktadha wa kitaifa na kimataifa ambao ulikuwa na nguvu na ulihitaji kuzingatiwa katika kazi yake.

Anasema, “Mienendo mingi ilijitokeza kuwa muhimu kwa wakati huo wa kisiasa na kiuchumi kwa Wakenya, kuhusiana na jukumu la Kamati ya Uongozi ambao ulitazamiwa na unatazamiwa bado kuleta haki na usawa miongoni mwetu.”

Katika kile ambacho kimesifiwa kama ishara ya uhuru wa Mahakama nchini Kenya, Agosti 20, 2021 Mahakama ya rufaa ilikubali uamuzi wa Mahakama Kuu kufuatia rufaa nne tofauti zilizotolewa na Rais Uhuru Kenyatta, Kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) Rt. Raila Odinga, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na sekretarieti ya kitaifa ya BBI.

Kwa kujibu, wabunge wanaoegemea upande wa Rais wakatarajia kupeleka ajenda ya marekebisho ya katiba Bungeni, baada ya kubainisha vifungu 52 katika mapendekezo ya BBI ambavyo wanasema havihitaji kura ya maoni kutekelezwa.

Kwa upande wake Raila Odinga, aliweka hadharani ukweli wake kwa kuukubali uamuzi wa Mahakama ya Rufaa, kama hatua mojawapo ya kusonga mbele katika kutekeleza lengo kubwa zaidi la kushughulikia maswala yanayokabili nchi.

Kauli hii inaendana na matukio ya hivi karibuni ya kisiasa yanayoonekana kuwa yanalenga kuweka msingi wa Urais wa Odinga, ikiwa ni pamoja na mikutano ya hivi karibuni ya kisiasa baada ya kuzinduliwa kwa kauli mbiu mpya ya Umoja tunaweza ya Azimio La Muungano (Umoja Unawezekana – Nia yetu ya kuunganisha watu wetu na nchi).

Hata hivyo majibu ya swali kuu la raia wengi nchini humo juu ya kupeana mikono na mapatano waliyoyafikia Kenyatta na Odinga yakajibiwa kwa vitendo ambapo mwanzo wa vuguvugu jipya la kisiasa na muungano umeonekana.

Mwanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi Mariam Martin ambaye anasomea shahada ya uzamili anasema hekima katika kuongoza Taifa inapaswa kuongozwa mbele kisha watu wanafuata na hii ilileta faraja kwani inaondoa sintofahamu ya kitakachotokea mbeleni hivyo ni lazima kuwa wamoja.

“Ile neno utu ambao ni mtu huja baadaye lakini maono ya Taifa yanapewa kipaumbele yaani Taifa kwanza tunatanguliza utaifa mbele halafu huyo mtu ajae baadaye maana ukitanguliza mtu ina maana kwamba aweza kujiamulia atakavyo na kujiamulia ni kuangamiza wengine,” amesema Mariam.

Kwa kauli kama hizi bila shaka tutashuhudia vinara wawili, Naibu wa Rais William Ruto na kiongozi wa muda mrefu wa upinzani Raila Odinga wakikabiliwa na kinyang’anyiro cha kumrithi Rais anayeondoka madarakani, Uhuru Kenyatta anayekamilisha muhula wake wa pili na wa mwisho uongozi.

Lakini, awamu hii ya uchaguzi inajiri wakati ambapo kuna hali ya kutoridhika kwa kiasi kikubwa kiuchumi, huku Wakenya wengi wakiwa na wasiwasi kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha, deni la umma na ufisadi uliokithiri na wakiona mabadiliko ya uongozi bila kujali matokeo jinsi yatakavyowajia.

Kwenye uchaguzi huu, yapo maswali matatu muhimu ambayo yametawala nchini humo moja likiwa ni nani atashinda vita vya kumrithi Kenyatta kama rais? na hii inatokana na kiongozi huyo kujitenga na naibu wake wa sasa ‘Ruto’ na badala yake kumuidhinisha mpinzani wake wa muda mrefu, Odinga.

Swali la pili, ni juu ya taasisi za uchaguzi nchini humo hasa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), je? zitakuwa na uwezo na uaminifu wa kusimamia uchaguzi unaoweza kuwa wa karibu na kuzuia dosari ambazo zimeathiri mizunguko miwili ya uchaguzi uliopita, na la tatu ni hali ya uchumi wa sasa wa nchi itaathiri vipi tabia ya ushiriki na upigaji kura?

Maswali haya yanatokana na changamoto kadhaa za mara kwa mara zinazokabili demokrasia ya Kenya, ambapo katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, nchi hiyo imeshuka katika suala la uimarishaji wa demokrasia.

Upande mmoja wa nchi unashuhudiwa na uwepo wa uhamisho wa mamlaka na mageuzi makubwa ya kitaasisi, ambayo ni muhimu zaidi kwa katiba mpya ambayo iligatua mamlaka kutoka kwa Serikali kuu hadi Serikali ndogo arobaini na saba na kuunda mifumo mpya ya kukuza uwakilishi wa kisiasa wa wanawake.

“Taifa letu lilianziasha mchakato wa kuwapa kipaumbele kina mama na hali hii inajidhihirisha baada ya kuona baadhi ya wanawake wapo katika nafasi nyeti kitaifa, na hii tunaiunga mkono kama tu jirani zetu Watanzania kwa sasa Rais ni mama, Spika pia ni mama bado Wizara nyingi wanaongoza akina mama hii ni safi sana,” anasema Mkenya Alice Macharia.

Ikumbukwe pia, Kenya imeepuka kwa kiasi kikubwa mwelekeo wa kurudi nyuma kidemokrasia kwa kuweka sera za uwazi ambazo zimeenea maeneo mbalimbali Duniani kote, ambapo baadhi ya Viongongozi wa nchi wameondoa ukomo wa muda wa kikatiba au kukandamiza vyama vya upinzani na kuingilia uhuru wa Mahakama.

Uchaguzi huu pia unaonyesha mipaka ya mwelekeo mzuri wa miungano ya wasomi iliyoanzishwa, kuondoa muingiliano wa kisiasa katika taasisi za serikali, na kushindwa kwa siasa za uchaguzi kuutoa utawala bora na uwajibikaji ambao huleta picha mbaya kwa demokrasia ya Kenya.

Katika vita hii ya kumrithi Kenyatta, inaonyesha kuwa siasa za Kenya zimesalia kuangaziwa na biashara zisizo imara za wasomi ambazo zinaweza kupunguza mgawanyiko wakati wa matatizo lakini pia kuendeleza ukosefu wa usawa na kudhoofisha uwajibikaji kwa matumizi mabaya ya mamlaka.

Mwanaharakati wa Kenya Deno Kipkirui yeye anasema, “Kuwa msomi haimaanishi kuwa mwanasiasa lakini siasa pia inahitaji wasomi ambao watatusaidia kuleta mageuzi na si kushibisha matumbo yao maana kenya ni ya wakenya wote na ni lazima wasomi wetu wawe na uzalendo kwa wakenya waache siasa za umimi na ukanda.”

Naye, Rurithi Francis mkazi wa Nairobi anasema “wasomi wana nafasi kubwa ya kuiendeleza Kenya lakini hicho kisiwe ni kibali cha kuwadharau watu wa chini kila wakipangacho wanapaswa kushirikisha watu wa chini yaani kila jambo liwe la ushirikiano hapo tutafika.”

Daniela Akina katika maoni yake anasema “Wakenya tunahitaji damu mpya, damu kubwa, tunahitaji mtu atakayejali watu yaani yule anayewajali Kenya sio kujijali wao wenyewe lakini haya yote ni siri yetu wenyewe ni chaguo la mtu binafsi tunaweka siri kwenye kura tu.”

Hata hivyo, mabadiliko makubwa ya chaguzi mbili zilizopita, yanaonesha kiongozi wa muda mrefu wa upinzani Raila Odinga anaingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi kama mgombeaji wa ukweli, akiungwa mkono na rais anayeondoka na viongozi wengi wa kisiasa nchini.

Kinyume chake, naibu wa rais aliye madarakani, William Ruto kwa miaka kumi iliyopita yeye ameendesha kampeni yenye mafanikio kutoka nje, akijinadi kama mbadala pekee anayefaa kuwa Rais anayefuata nchini Kenya kumrithi Rais anayemaliza muda wake Uhuru Kenyatta.

Kenyatta alishinda urais kwa kuunda muungano kati ya msingi wake wa jadi wa eneo la kati la Kenya na ngome za Ruto katika Bonde la Ufa, huku Odinga, ambaye chama chake cha Orange Democratic Movement (ODM), yeye akiongoza muungano wa upinzani wa vyama vidogo vilivyoko katika mikoa ya magharibi na pwani ya Kenya.

Odinga hata hiyo, alipinga uhalali wa chaguzi zote mbili akidai kuna kasoro nyingi na hii ni ilitokana na uamuzi ulioamriwa na Mahakama wa kufanya marekebisho katika mchuano huo wenye mgogoro wa 2017, ambapo alitoa wito kwa wafuasi wake kususia kura na kukataa kutambua ushindi wa Kenyatta.

Katika kuongezea mawazo katika hili, Mwanasheria Alex Kiambi wa Kericho anasema “Hatua hii ilifanya nchi kujikuta ikiwa katika mgawanyiko wa kisiasa, kikabila, na kikanda, na kusababisha hofu ya ghasia, kama ambavyo mzozo mkubwa wa uchaguzi uliotokea wa 2007.”

Aina ya siasa za sasa nchini Kenya tangu kuanza kwa kipindi cha mpito cha nchi kuelekea demokrasia ya vyama vingi mwanzoni mwa miaka ya 1990, ushindani wa uchaguzi kwa ujumla umejikita katika miungano lege inayozingatia viongozi binafsi wa kisiasa, ambao wana matumaini ya kupata kura kutoka kwa ngome zao za kikabila.

Matumaini haya pia yanatokana na kubadilishana nyadhifa za kisiasa ikiwemo ufikiaji wa rasilimali za serikali ikizingatiwa kwamba hakuna kabila hata moja linalofurahia wingi wa kura huku kukiwa na udhaifu katika utekelezaji wa shughuli zinazowagusa moja kwa moja Wananchi.

“Viongozi wa kisiasa mara nyingi hupata mamlaka kupitia mazungumzo ya kibinafsi yanayofanywa bila ya faragha na miungano ya huvunjika pindi wanapotimiza madhumuni yao ya uchaguzi, kama ilivyojionesha hivi majuzi kwa Chama cha Jubilee,” anasema raia wa Kenya Mangari Warende.

Hata hivyo chaguzi zijazo pia zinaangazia mipaka ya mantiki hii ya siasa hasa zile za muungano zinazodhohofisha ushirikishwaji wa kidemokrasia kwa wasomi wa kisiasa mara kwa mara wameegemea kwenye mazungumzo ya ndani kuchagua wagombeaji wa nyadhifa muhimu zilizochaguliwa na kutumia mbinu za kugawa maeneo ili kuepuka kuwa na wagombea kushindana wao kwa wao.

Wangari Warende anasema “Zipo njia tofauti za kutathmini mwelekeo wa kidemokrasia wa Kenya kwa kuweka viongozi wanaowajibika na kuimarisha utawala bora ambapo Wakenya wengi wana shauku ya kuhakikisha hakuna vikwazo vitakavyojitokeza katika mchakato mzima wa uchaguzi, bila kujali matokeo ya kura ya Agosti 2022.”

Anaendelea kufafanua kuwa “Wapiga kura wengi wana wasiwasi wa kutokea upya kwa ghasia ambazo zinaweza kudhoofisha zaidi uchumi wa nchi na uwezekano wa kusababisha mabadiliko ya kisiasa huku wakidhani kwamba masuala ya kijamii, kiuchumi na madai ya suluhu huenda yakatawala kabla na baada ya uchaguzi.”

Kutokana na madai ya Warende na wananchi waliotoa maoni yao akiwemo Mwanasheria Alex Kiambi, huenda wapigakura wengi wakajitokeza ili kuwaadhibu viongozi ambao wanahisi hawakutekeleza ahadi zao, na kusababisha wengi wao kuwa katika hali mbaya ya kiuchumi baada ya kupanda kwa gharama za maisha.

Hatua hii inatoa changamoto kwa kiongozi ajaye ambaye ana kazi ya kuhakikisha anarejesha hali ya kawaida ya kiuchumi kwa wananchi wake ambao kwasasa wanalia na ugumu wa maisha licha ya kwamba hali waliyonayo imezikumba jamii nyingi za nchi za bara la Afrika na Dunia kwa ujumla.

Hata hivyo, macho na masikio ya watu wengi yapo nchini Kenya, waangalizi wa uchaguzi mbalimbali pia wapo wakiwemo wale wa kutoka umoja wa ulaya pia wapo nchini humo, lengo ni moja tu kuhakikisha wanaangalia mchakato mzima utakavyoendelea mpaka atakapotangazwa mshindi.

Waafrika walio wengi bila shaka wanaiombea Kenya na kuwataka wenye mamlaka kuhakikisha hakuna ghasia wala machafuko ya aina yeyote kabla na baada ya uchaguzi, ili kuleta amani miongozi mwa Wakenya Taifa ambalo lina wakazi anaohitaji usawa na amani sawa na Mataifa mengine Duniani.

Umeme Vijijini kuchochea mabadiliko kiuchumi
Jonas Mkude amfagilia Kocha Zoran Maki