Uchaguzi wa kumpata Meya wa jiji la Tanga umezua vurugu kubwa muda mfupi uliopita baada ya Mkurugenzi wa Jiji hilo kumtangaza mgombea wa CCM kuwa mshindi licha ya chama hicho kuzidiwa idadi na madiwani wa Chama cha Wananchi (CUF).

Madiwani wa Ukawa wako 20 huku madiwani wa CCM wakiwa 17, hivyo upande wa UKAWA walikuwa na imani kuwa kwa wingi wao wangeweza kuongoza Halmashauri hiyo kwa kupata kura nyingi.

Taarifa za kuaminika kutoka katika chumba cha kupigia kura zimeeleza kuwa baada ya zoezi la kupiga kura, Mkurugenzi na timu yake walihesabu kura zote zilizopigwa na baadaye alitangaza kuwa mgombea wa CCM ameshinda kwa kupata kura 19 dhidi ya mgombea wa CUF ambaye amepata kura 18.

Baada ya tangazo hilo, vurugu kubwa ilizuka ukumbini hapo huku CUF wakidai kuwa ilikuwa mbinu ya CCM kumtumia Mkurugenzi wa jiji hilo kuhujumu uchaguzi na kumpa ushindi mgombea wake.

Zoezi la kumchagua Meya wa jiji hilo lilitanguliwa na uchaguzi wa Naibu Meya ambapo mgombea wa CUF alitangazwa kuwa mshindi kwa kupata kura 21 dhidi ya mgombea wa CCM aliyepata kura 16, matokeo ambayo CUF wanadaiwa kuyapinga wakidai yaliandaa mazingira ya hujuma ya Meya.

“CUF wanadai kuwa Mkurugenzi aliandaa mazingira ili ionekane kuwa kuna diwani mmoja wa CCM alimpigia kura mgombea wa CUF kwenye unaibu Meya, ili baadae aoneshe kuwa kuna wagombea wa CUF waliompigia kura mgombea wa CCM na kumuwezesha kushinda,” Chanzo kimeiambia Dar24.

 

Tanesco waanika kiasi wanachomdai Wema Sepetu Kwa Wizi wa Umeme
Jerry Muro Kufikishwa Mbele Ya Kamati Ya Maadili