Baada ya siku takribani 52 tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha atangaze kufuta matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu, Jaji Mark Momani amejitokeza na kueleza kushangazwa na uamuzi huo.

Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Jaji Bomani alieleza kushangazwa na tangazo la Jecha ambalo alidai halikutoa ufafanuzi wa kisheria na kifungu cha sheria kinachompa mamlaka hayo.

“Mimi mwenyewe nashangaa, je kwa nini uchaguzi ulifutwa? Lakini Mwenyekiti wa ZEC wakati akitangaza kuufuta hakubainisha kifungu chochote cha sheria kinachomuwezesha kufuta na ndio maana baada ya kutangaza baadhi ya wajumbe walipinga,” Jaji Bomani alisema.

Jaji Bomani ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa kwanza wa serikali, aliongeza kuwa mazungumzo yanayoendelea hivi sasa yanaweza yasizae matunda mema endapo pande zote mbili hazitajikita katika sheria na katiba ya nchi.

Alipendekeza kuundwa kwa jopo litakalohusisha Jaji Mkuu na wajumbe wa jumuiya za kimataifa ili kufanya uchunguzi kubaini kama kasoro zilizojitokeza kwenye uchaguzi huo zinaweza kupelekea uchaguzi huo kufutwa. Alisisitiza kuwa ili hilo lifanikiwe, lazima vyama vyote viwe tayari kukubali matokeo ya uchunguzi wa jopo hilo.

Hata hivyo, Jaji Bomani alimshauri mgombea urais ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuridhia kurudiwa kwa uchaguzi huo kwa kuwa watu waliompigia kura awali ndio wale ambao watakaompigia tena.

 

Ukosefu wa Madarasa wazuia Wanafunzi 12,225 kuingia kidato cha Kwanza Dar
Mnyika hajaridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Waziri wa Maji, Aomba Waziri Mkuu Aingilie Kati