Hii ni mara ya pili narudi kwenye tovuti hii kuchambua wimbo wa Ali Kiba, mara ya mwisho ilikuwa mwaka jana aliposhusha kombora la nyuklia la ‘Seduce Me’. Kombora hilo wengi hawakulipata vizuri, lakini sumu yake taratibu iliwaingia na wakanyoosha mikono kukubali utawala wa ‘King Kiba’ kwenye Bongo Fleva.

Juzi, Ali Kiba na timu yake ya Rock Star 4000 ambayo sasa ni ‘Rock Star Africa’, waliamua kuachia kwa mkupuo audio na video ya ‘Mvumo wa Radi’, kwa lengo la kuikata kiu ya takribani mwaka mzima ya mashabiki waliokuwa kwenye foleni wakisubiri japo tone la sauti ya Kiba.

Ikiwa tayari zinakaribia saa 72 zitakazokamilika leo, swali ambalo lipo kwa wengi ni Je, Ali Kiba amefanikiwa kuikata kiu ya mashabiki wake? Je, amepatia au la…!

Ikiwa tayari video yake imeangaliwa zaidi ya mara 781,150 ikivuta comments zaidi ya 7,300 zenye mitazamo tofauti na ‘utimu ukiwa humohumo’, nimeona niipitie kidogo na kuidadavua. Hadi sasa inashika nafasi ya kwanza, Trending (gumzo).

Kwanza kabisa, nilipousikiliza huu wimbo hadi mwisho, sikuelewa kwa haraka, hivyo ilinipasa kurudia tena. Kwa bahati nzuri nilikuwa nasikiliza na watu wengine wawili ambao kabla ya kuusikiliza, tukiwa na kiu sekunde chache baada ya kumsikia Clouds FM kuwa anauweka YouTube, tulikubaliana hakuna ‘U-Team’.

Baada ya kuusikiliza, wa kwanza niliyemuona alikuwa kama kapigwa na mshangao lakini hakusema kitu japo sura yake iliongea kwa niaba yake. Wa pili nikaona kama anataka tuurudie tena, anasema ‘hakutegemea’. Hakutegemea nini?

Nikafanya nao mjadala baada ya kuuangalia YouTube mara tatu huku views zikiongezeka kwa kasi. Ni kama watu lukuki walikuwa kwenye foleni.

Kupitia mjadala ule nilijifunza mengi na mimi nikawa na mengi. Kwanza, kwa wanaomfahamu vizuri Ali Kiba, hakuwashangaza. Anayesikika kwenye ‘Mvumo wa Radi’ ndiye King Kiba ninayemfahamu mimi. Yaani huyu ndiye Kiba wa ‘Dushelele’, ‘Usiniseme’, ‘Mwana’ n.k. Ali Kiba anayepita njia yake wakati ambapo wasanii wengine wanakuwa kwenye msafara mmoja wa aina fulani ya muziki.

Ukiangalia sasa hivi, nyimbo nyingi zinafanana na miondoko ya wasanii wa Nigeria, yaani mimi huziita ‘Tekno Syndrome’. Lakini Kiba ameamua kupita njia yake akizichanganya Bongo Fleva na Dansi/Rhumba.

Ubora wa sauti ya Ali Kiba hauna pingamizi kwenye ‘Mvumo wa Radi’. Mpangilio mzuri wa sauti zilizosikika na uimbaji ni kiwango cha kutaka kuihakikishia dunia yeye sio msanii tu bali ni mwimbaji ‘specifically’. Kiwango cha uimbaji kiko kwenye kipimo cha juu zaidi cha Bongo Fleva na Dansi.

Huyu ndiye Ali, ‘the best vocalist wa project ya One 8 iliyosimamiwa na R-Kelly.

Production/utayarishaji:

Man Walter, Man Maji. Huyu jamaa anastahili heshima yake ya kuwa wa kipekee na anayejua kama chakula kweli kimeiva kabla ya kukipakua. Vyombo vilivyosikika kwenye ‘Mvumo wa Radi’ ni vya kibabe. Kila chombo kinaimba na kinasikika kwenye mstari wake bila kuingilia chombo kingine, yaani unaweza ku-feel kuwa hili ni gitaa linapiga nini… utaisikia ‘baseline’ inavyopita, ngoma na vingine. Ni kama Man Walter amempendelea tena Ali Kiba, uzalishaji huu unanikumbusha Dushelele lakini uko juu ya Dushelele. Uchanganyaji wa sauti ni wa kipekee. Uko mahala pake na unadhibitisha kuwa umepita kwenye mikono salama ya mtayarishaji mwenye uzoefu.

Ujumbe:

Hapa kwenye ujumbe ndipo kwenye mengi yanayoweza kuwaumiza vichwa wachambuzi. Kwanza ujumbe hauna maneno tata, ni ujumbe wa moja kwa moja. Kiba anataka penzi lake na Amina Rikesh livume kama radi. Mvumo wa radi huwa hauishii ndani, huleta athari hata kwa watu wengine wa eneo hilo.

Ndio maana Ali Kiba anahama na kuwaeleza waafrika wote kuwa ‘Tupendane’, akitaja nchi kadhaa ikiwemo Kenya alikofika yeye na kumpenda ‘kwelikweli’ mtoto wa Mombasa. Watu wanauliza kwanini Kiba alihamia ‘Afrika tupendane, mara atampenda mama, baba yake na ndugu zake? Kwa ufupi huu ni wimbo wenye ujumbe wa mapenzi ya kiutu uzima, penzi lenye mvumo wa radi ambalo Ali Kiba anajaribu kufikisha ujumbe wake… penzi hilo likivuma kama radi lazima utampenda mama kizaa chema, baba na ndugu zake.

Tumekuwa tukiona mfano wa mapenzi ambayo hayana mvumo wa radi, ambayo wapendanao huwalaumu mawifi, shangazi na hata wazazi kwa kuwaingilia. Lakini linalovuma kama radi, litawasomba pia ndugu na hata bara zima litafikiwa na mapenzi yatakuwa kila sehemu.

Kama wewe ni mchambuzi mzuri wa mashairi, unaweza kuelewa namna ambavyo amejaribu kufikisha jumbe mbili kwa mpigo.

Changamoto/Mapungufu

Kwanza, kwakuwa wimbo huu haujakaa kwenye mkondo wa nyimbo zinazovuma hivi sasa, utapokelewa kwa hisia tofauti sana. Wapo ambao hawatauelewa kabisa kabisa hata kama ni mashabiki wake. Yaani, huenda walitegemea ‘Seduce Me’ nyingine. Wanachokutana nacho ni tofauti kabisa.

Video ya wimbo huu ni nzuri, ina ubora mzuri sana. Muonekano wa Kiba pia na hasa kipande cha igizo fupi lilolowakumbusha pia kipaji kingine cha King Kiba cha uigizaji. Ndiyo, Ali amewahi kuigiza kwenye Bongo Movie na moja ya filamu alizofanya ni ‘Mrembo Kikojozi’.

Lakini, kama wasemavyo wengi, Ali Kiba angewapa nafasi pia timu ya madansa wafanye yao ili kukoreza joto la shangwe ya Dansi/Rhumba.

‘Mvumo wa Radi’ unaweza usiwe wimbo utakaokimbia kwa haraka kama ‘Seduce Me’, lakini sumu yake itaingia taratibu kwenye masikio ya wengi na tutaanza kuuimba. Lakini utapata ukosoaji wa hali ya juu.

Wimbo huu pia utatoa picha halisi ya ‘kutotabirika’ kwa Ali Kiba. Usimtegemee atarudi vipi, ni kama miguu ya Lionel Messi, huwezi jua upi utakaopachika goli. Kupitia ‘Mvumo wa Radi’, watu wa rika zote wamewekwa pamoja.

Magaidi walipua makanisa matatu kwa mpigo
Kingwangalla akabidhi magari 6 kwa wabunge

Comments

comments