Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA huenda likafanya maamuzi ya kuandaa michuano mingine itakayohusisha vilabu vya nchi wanachama tofauti na ligi ya mabingwa barani Ulaya pamoja na Europa league.

Taarifa za ndani ya shirikisho hilo zinadai kwamba, tayari wazo wa kuanzishwa kwa michuano hiyo limeshawasilishwa kwa wajumbe wa kamati ya utendaji na wakati wowote litaanza kufanyiwa kazi.

Nchi wanachama wa UEFA ambao wapo 54, wameshakubaliana kwa pamoja juu ya kuanzishwa kwa michuano hiyo, na sasa wanasubiri kama wazo lao litapitishwa na kamati ya utendaji ya shirikisho hilo, kabla ya kurejeshwa kwao na kupigiwa kura ya ndio ama hapana.

Michuano hiyo inayopigiwa upatu kuanzishwa na UEFA itatoa nafasi ya kushirikisha klabu ambazo zitakua zinakosa nafasi ya kuendelea kwenye michuano ya Europa League ambayo huchezwa katika hatua tatu tofauti.

Pendekezo lililopo kwa sasa ni kuona michuano hiyo inaanza kuchukua nafasi yake barani humo kuanzia mwaka 2018.

Mtendaji mkuu wa shirikisho la soka nchini Ukraine, Volodymyr Geninson, amezungumza na vyombo vya habari na kusema anaamini wazo hilo litapatiwa baraka na uongozi wa juu wa UEFA na litaanza kufanyiwa kazi kwa vitendo.

Amesema lengo kubwa ni kutaka kuona klabu za soka barani Ulaya zinapata wigo mkubwa wa kushindana hata kama zitakua zimeshindwa kuendelea kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya pamoja na Europa League.

Kutolewa kwa wazo hilo, kunaendelea kuonyesha ni vipi shirikisho la soka barani Ulaya linavyojipanga kulisaidia soka la barani humo kwa kubuni michuano mbalimbali ambayo itashirikisha washiriki wengi kwa wakati mmoja.

Kama itakumbukwa vyema, tayari rais wa UEFA Michel Platini ameshaungwa mkono katika wazo lake la kutaka timu shiriki kwenye fainali za mataifa ya barani Ulaya kuongezwa na kuanzia mwaka 2016 mpango huo utaanza kutekelezwa, huku kipengele kingine kilichopitishwa na UEFA ni kubadili mfumo wa kuchezwa kwa fainali hizo kuanzia mwaka 2020.

Kuanzia mwaka huo UEFA itashuhudia fainali za mataifa ya barani Ulaya zikichezwa katika bara zima kwa kushirikisha miji iliyoshinda tenda ya kuwa wenyeji.

Kapuya Ajitetea Kwa Magufuli Kuhusu Lowassa
Magufuli Ajivisha Joho La Kampeni Ya Chadema