Mameneja wa klabu kubwa barani Ulaya wamelitaka shirikisho la soka barani humo (UEFA) kuitazama upya sheria ya goli la ugenini na ikiwezekana kuiondoa kabisa katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya na ile ya Ueropa League, ili kuleta usawa katika ushindani.

Ombi lingine lililowasilishwa na mameneja hao ni kutaka shirikisho hilo kubadilisha kanuni za muda wa kufungwa kwa dirisha la usajili barani Ulaya, ili uendane sambamba na tarehe za mwisho katika nchi wanachama.

Kaimu katibu mkuu wa UEFA, Giorgio Marchetti amethibitisha kupokea taarifa ya maombi hayo na amethibitisha itajadiliwa kwenye mkutano mkuu wa mameneja, ambao utafanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Mkutano huo wa mwaka utawashirikisha mameneja kama Massimiliano Allegri (Juventus), Carlos Ancelotti (Napoli), Unai Emery (Arsenal), Paulo Fonseca (Shakhtar Donetsk), Julen Lopetegui (Real Madrid), Jose Mourinho (Manchester United), Thomas Tuchel (Paris St Germain) na aliyekua meneja mkuu wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger.

“Mameneja wamekaa na kutafakari kwa kina, wameniandikia kuhusu sheria ya bao la ugenini ili iweze kufanyiwa marekebisho, tumewapa nafasi ya kulijadili tena hilo, kabla ya kufikishwa kwenye mkutano mkuu wa UEFA,” Marchetti aliwaambia waandishi wa habari.

“Hapa tunaangalia namna ya kuliboresha soka la Ulaya, ndio maana tumetoa nafasi kwa mameneja kulijadili suala hilo katika kikao chao kwa mara nyingine tena, tunaamini watatoka na jibu imara zaidi ambalo litawezesha sababu kadhaa kuelekea mkutano mkuu wa UEFA.”

Sheria ya bao la ugenini kwa mara ya kwanza ilianza kutumika katika michuano ya kombe la washindi barani humo (European Cup Winners) mwaka 1965, ambayo kwa sasa ndio michuano ya ligi ya mabingwa.

Hata hivyo endapo maamuzi ya mameneja yataridhiwa na kupitishwa na shirikisho la soka barani humo, bado sheria haitoweza kutumika kwa msimu huu wa 2018/19, na badala yake huenda ikaanza kutuika kuanzia msimu ujao.

Kuhusu sheria ya kubadilishwa kwa tarehe ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi, kaimu katibu mkuu wa UEFA amesema mameneja hao wametaka nchi kadhaa kuiga mfumo wa ulioanza kutumiwa na  chi za England na Italia kwa msimu huu wa 2018/19.

Sheria ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi kwa nchi hizo ilianza kutumika, kwa dirisha kufungwa katikati ya mwezi Agosti, tofauti na ilivyokua misimu iliyopita, ambapo dirisha lilikua likifungwa mwishoni mwa mwezi huo.

Bado nchi za Hispania, Ujerumani na Ufaransa zimeendelea na mfumo wa kufungwa kwa dirisha la usajili mwishoni mwa mwezi Agosti kama ilivyoagiza sheria ya shirikisho la soka barani Ulaya UEFA.

“Wamekua na mawazo tofauti kuhusu jambo hili, pia tumewapa nafasi ya kulijadili tena, na watakapotoka na majibu sahihi yatakayokua na sababu za kulipeleka kwenye mkutano mkuu, tutafanya hivyo ili kuleta mabadiliko yenye ustawi katika soka la barani kwetu, Marchetti anakaririwa.

LIVE: Rais Magufuli katika uzinduzi wa barabara ya Simiyu mjini Musoma
Sauti ya Hamisa yaibua makubwa ya Wema, Mange avujisha siri nzito