Kufuatia mvutano kuhusu uhalali wa uenyekiti wa Profesa Ibrahim Lipumba ndani ya Chama Cha Wananchi (CUF), Mahakama Kuu imewapa siku 7 mwanasiasa huyo pamoja na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kujibu hoja dhidi yao.

Jaji wa Mahakama Kuu, Sekieti Kihiyo jana alitoa muda huo kwa walalamikiwa hao kujibu madai yaliyowasilishwa na Bodi ya Wadhamini wa chama hicho dhidi yao.

Katika kesi ya msingi iliyofunguliwa mahakamani hapo na Bodi hiyo wa Wadhamini ya CUF, walalamikaji hao wanaiomba mahakama kutoa amri ya kubatilisha barua ya Msajili inayomtambua Profesa Lipumba kama Mwenyekiti wa halali wa chama hicho.

Bodi hiyo ya Wadhamini pia imeiomba mahakama kutoa amri ya kumzuia Msajili kuingilia utendaji wa ndani wa chama hicho.

Profesa Lipumba aliandika barua ya kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu nafasi ya Uenyekiti wa chama hicho aliouchukua baada ya chama hicho kumkaribisha Edward Lowassa kuwa mgombea anayeungwa mkono na Ukawa.

Msajili wa vyama vya siasa aliandika barua akieleza kumtambua Profesa Lipumba kama Mwenyekiti halali wa chama hicho ikiwa ni siku chache baada ya uongozi wa chama hicho kutangaza kumfuta uanachama.

Video: 'Kama Trump amefanikiwa, basi nchi inafanikiwa' - Obama
Video: Ombi la Makonda kwa Rais Magufuli wakati wa kuaga mwili wa Samuel Sitta