Wananchi nchini Ufaransa wako kwenye hatari dhidi ya hali mbaya ya hewa baada ya kuvunja rekodi ya kiwango cha juu cha joto ikiwa na nyuzi joto 45.9.

Kiwango hicho kimetangazwa leo wakati ambapo bara la Ulaya linakabiliwa na tatizo la kuwa na kiwango cha juu cha joto kinachotishia maisha.

Waziri wa Afya wa Ufaransa, Agnès Buzyn amesema kuwa kutokana na hali hiyo kila mmoja yuko kwenye hatari kubwa. Kiwango kipya cha joto kimepimwa katika mji wa Gallargues-le-Montueux. Kabla ya mwaka huu, kiwango cha juu zaidi kilichowahi kurekodiwa ni nyuzi joto 44.1 cha mwaka 2003 ambacho kilisababisha vifo vya maelfu ya watu.

Mamlaka ya hali ya hewa ya Ufaransa imetoa tahadhari kwa wananchi wake ikieleza kuwa kuna hatari ambayo haiwezi kutabiriwa hususan katika eneo la kusini mwa nchi hiyo.

Eneo la kusini la bara la Ulaya limekumbwa na hali hiyo mbaya ya joto. Ujerumani, Ufaransa, Poland na Jamhuri ya Czech ni nchi ambazo zimerekodi kiwango cha juu zaidi kuwahi kutokea katika mwezi Juni.

Serikali ya Italia kupitia Wizara ya Afya imetangaza hali ya dharura kutokana na kiwango cha juu cha joto kwenye majiji 16.

Utafiti: Unywaji wa kahawa unapunguza uzito
Sababu ya kasi ya ugonjwa wa TB nchini yawekwa wazi

Comments

comments