Ronda Rousey amekumbwa na dhahba ya kipigo kikali asichotegemea kutoka kwa mwanamke wa shoka wa Brazil, Amanda Nunes katika pambano lao lililomalizika mapema leo.

Katika hali ambayo wengi hawakuitegemea, Nunes amemchapa Rousey katika sekunde ya 48 ya raundi ya kwanza ya pambano kwa Makonde mfululizo yaliyomfanya muamuzi kuingilia kati kumuokoa bingwa huyo wa zamani wa dunia wa ‘bantamweight’.

Nunes amedhihirisha kuwa yeye ni ‘Simba’ kweli kama anavyojiita ikiwa ni miezi michache tangu alipomchapa Holly Holm ambaye awali alivuruga rekodi ya Rousey ya kutopigwa. Hivyo, Nunes ameibuka kuwa ‘kiboko yao’ kwa kuwashinda wababe hao kwa nyakati tofauti.

“Kabla hatujatoka nje nilizungumzia wakati huu kuwa ni wakati wangu. Alikuwa na wakati wake. Alifanya mengi kwenye mchezo huu. Asante Ronda Rousey…. Mimi ndiye bingwa sasa, Simba!” Nunes alisema baada ya kupata ushindi huo.

Aliongeza kuwa ingawa anajua watu wanampenda sana Rousey, yeye aliomba pambano hilo akiwa anajua atakachofanya. Alitamba kuwa alijiandaa kiakili na kiroho kwa sababu alijua Rouse ni mzuri zaidi.

Kwa tambo, aliwataka watu wasahau kabisa kuhusu Rousey, “hakuna mtu atakayechukua mkanda huu kutoka kwangu.”

JPM kushiriki mkesha mwaka mpya uwanja wa uhuru
Ewura wapandisha bei ya umeme