Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Miraji Athuman Madenge, huenda akaibuka kinara wa upachikaji mabao kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, itakayofikia tamati leo Jumatano (Januari 13) mjini Unguja visiwani Zanzibar.

Mpaka sasa mshambulaiji huyo ambaye amepata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyoanza juma lililopita, ameshafunga mabao manne.

Miraji alifunga mabao hayo kwenue mchezo dhidi ya Chipukizi FC akifunga mabao mawili kati ya matatu yaliyoipa ushindi Simba SC, akafunga tena bao moja kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar waliokubali kichapo cha mabao mawili kwa sifuri na kisha akafunga kwenye mchezo dhidi ya Namungo FC waliolala kwa mabao mawili kwa moja.

Mchezaji anayemfuata kwa karibu katika mbio hizo za kuwania ufungaji bora wa Kombe la Mapinduzi ni mshambuliaji mwenza wa Simba, Meddie Kagere pamoja na Steven Sey wa Namungo FC ambao kila mmoja amezifumania nyavu mara mbili.

Miraji anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Simba SC kitakachopambana dhidi ya Young Africans, baadae hii leo Uwanja wa Amaan, kisiwani Unguja-Zanzibar.

Wakati huo huo kuelekea mchezo dhidi ya Young Africans, Simba SC itawakosa baadhi ya wachezaji wake ambao wameitwa kwenye timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayoendelea kujiandaa na Fainali za Mataifa bingwa Barani Afrika (CHAN) zitakazorindima nchini Cameroon baadae mwezi huu.

Wachezaji hao ni Aishi Manula, John Bocco,Erasto Nyoni, Shomari Kapombe na Said Ndemla huku kiungo Jonas Mkude akiendelea kutumikia adhabu ya kusimamishwa kufuatia utovu wa nidhamu.

Mshambuliaji Charles Ilanfya hayupo fiti kwa kuwa hajacheza mchezo hata mmoja wa Kombe la Mapinduzi msimu wa 2021, huku beki kutoka Ivory Coast Pascal Wawa akiwa hana hali nzuri kiafya.

Hata hivyo tetesi zinaeleza kuwa huenda Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Seleman Matola akawatumia Clatous Chama, Luis Miquissone, Rarry Bwalya ambao walipewa mapumziko baada ya mchezo wa kimataifa dhidi ya FC Platinum.

Chadema yakana kufungua kesi ICC
Odinga: Urais uwe wa makabila Kenya