Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amemtumia ujumbe maalumu Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli unaoelezea msimamo wa Serikali yake kuhusu kukerwa na matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Mbunge wa jimbo la Starehe, Charles Njagua Kanyi maarufu kwa jina la Jaguar.

Ujumbe huo umewasilishwa na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dany Kazungu na kupokelewa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Dkt. Magufuli, ofisini kwa Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar Es Salaam.

Akipokea taarifa hiyo Waziri Mkuu amesema kuwa Watanzania wamefurahishwa na hatua mbalimbali zilizochukulia na Serikali ya Kenya dhidi ya mbunge huyo zinazodhihirisha kwamba matamshi hayo hayakuwa msimamo wa Serikali ya Kenya wala wananchi wake bali ulikuwa ni msimamo binafsi wa mbunge huyo.

Amesema kuwa siku zote Watanzania na Wakenya wamekuwa huru kuishi na kufanya kazi au biashara katika nchi za Afrika ya Mashariki na pale yalipotokea matatizo au kutokukubaliana serikali husika hukaa mezani na kumaliza tofauti hizo.

“Uhusiano kati ya Kenya na Tanzania ni wa karibu mno na wa kindugu kwani kuna baadhi ya makabila yapo katika nchi mbili hizi kama vile Wamasai na Wakurya na Wajaluo, hivyo ushirkiano katika masuala ya mbalimbali yakiwemo ya kabiashara na ya kijamii haukwepeki,”amesema Majaliwa

Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa viongozi na wananchi wa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kujiepusha na kauli zenye viashiria vya kujenga chuki, uhasama na migongano miongoni mwa wananchi kwani kauli hizo zisipodhibitiwa mapema zinaweza kusababisha hofu na kutokuelewana miongoni mwao.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania kuendelea kuishi kwa amani na upendo na ndugu zao wa Kenya na wageni wote kutoka nchi za Afrika ya Mashariki na duniani kwa ujumla ambao wapo nchini wakifanya shughuli mbalimbali kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Mambo yetu yote katika nchi za Afrika ya Mashariki hasa ya biashara na ya kiuchumi kwa ujumla yataenda vizuri endapo tutalinda na kudumisha amani, bila amani tutaogopana na tutashindwa kabisa kushirikiana,” amesisitiza Majaliwa.

Hata hivyo, ameahidi kuwa Serikali ya Tanzania kamwe haitaruhusu wala kufumbia macho kauli au vitendo vyovyote vyenye viashiria vya uchochezi dhidi ya nchi jirani ili kulinda na kuunga mkono juhudi mbalimbali za ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi zinazofanywa na viongozi wakuu wa Mataifa ya Afrika.

Kwa upande wake Balozi Kazungu amemshukuru Waziri Mkuu kwa kauli yake aliyoitoa Bungeni jijini Dodoma iliyowataka Watanzania kuwa watulivu na wayachukulie matamshi ya Mbunge wa jimbo la Starehe nchini Kenya, Njagua kuwa ni msimamo wake binafsi na siyo msimamo wa Wakenya na Serikali yao.

Balozi Njagua mesema Msimamo wa Rais Kenyatta siku zote umekuwa ni kuwapokea na kuwakubali ndugu zao wote wanaotoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki walioamua kuishi au kufanya biashara nchini Kenya.

Membe amkalia kooni Musiba, 'Wamenichafua sana'
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 3, 2019