Waziri wa Afaya, Ummy amesema takwimu za Shirika la Afya Duniani za mwaka 2018 zinaonyesha kuwa kuna wanawake takribani millioni mbili (2,000,000) wanaoishi na Fistula Duniani kote, Inakadiriwa kuwa wagonjwa wapya kati ya 50,000 na 100,000 hupatikana kila mwaka, wakati juhudi za kutibu Fistula ulimwenguni kote huishia kutibu wagonjwa 20,000 tu.

Kwa upande wa Tanzania, Waziri Ummy amesema inakadiriwa kuwa na wanawake takribani 2500 ambao wanapata fistula kila mwaka, huku idadi ya wanaopatiwa matibabu ikiwa ni takribani wanawake 1,000 na kuongeza kuwa Tanzania imepiga hatua katika matibabu haya.


Aidha, Waziri Ummy ametaja takwimu zinazoonyesha kuwa idadi ya Wanawake wanaojitokeza kutibiwa Fistula kwenye Hospitaii za CCBRT, Bugando, Nkinga na Kuvulini Maternity Center imepungua kwa zaidi ya 30% kuanzia mwaka 2015 mpaka 2019.

Mwaka 2015, wanawake 1337 walipatiwa matibabu ya Fistula, Mwaka 2016 walikuwa 1356, mwaka 2017 idadi hiyo ikashuka na kufikia 1060, mwaka 2018 ikashuka tena na kufikia idadi ya wanawake 900, na mwaka 2019 ikashuka zaidi na kufikia wanawake 852.

Amesema hii imetokana na kuimarika kwa huduma za Afya ya mama wajawazito ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma za upasuaji wa dharura chini ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli.

“Mama mjamzito endapo atawahi kliniki mapema kwa ajili ya uchunguzi wa maendeleo ya afya yake na mtoto na kuhakikisha anajifungulia katika kituo cha kutolea huduma za afya atapunguza uwezekano wa kupata tatizo la Fistula.

“Nitumie fursa hii kuendelea kuhimiza akina mama wajawazito kuwahi kliniki mapema, kukamilisha mahudhurio yote manne na kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za Afya”. Ameongeza Waziri Ummy.

Hayo yamesemwa leo na Waziri, Mwalimu wakati akiongea na Waandishi wa Habari katika kuadhimisha siku ya Fistula duniani inayoadhimishwa tarehe 23 Mwezi Mei kila Mwaka, yenye kauli mbiu mwaka huu inayosema “Tokomeza unyanyasaji wa kijinsia: Tokomeza huduma ya afya isiyo na usawa; Tokomeza Fistula sasa!

Dubai kufunga biashara miezi 6 kutokana na Covid 19
Ndege yaanguka kwenye makazi ya watu Pakistan