Waziri Mkuu, Theresa May ameungwa mkono na baraza lake la mawaziri kuhusiana na rasimu ya makubaliano kati ya serikali yake na Umoja wa Ulaya, juu ya masharti ya Uingereza kujiondoa ndani ya umoja huo ifikapo Machi 2019.

Katika taarifa fupi aliyoisoma kwa vyombo vya habari baada ya kukubaliana na mawaziri wake, May amesema kuwa ana imani thabiti kwamba rasimu ya makubaliano ya kuondoka katika Umoja wa Ulaya ndio muafaka bora zaidi ambao ungeweza kufikiwa baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya.

Kizingiti kikubwa katika majadiliano juu ya mchakato wa Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya, maarufu kama Brexit, kilikuwa juu ya mpaka kati ya Jamhuri ya Ireland ambayo inaendelea kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, na Ireland ya Kaskazini, sehemu ndogo iliyopo Kaskazini mwa kisiwa cha Ireland, ambayo ni himaya ya Uingereza.

Aidha, rasimu hiyo ya makubaliano kuhusu Brexit inaruhusu kipindi cha mpito cha miezi 21 kitakachoanza baada ya Uingereza kuondoka rasmi katika Umoja wa Ulaya, na kipengele cha kuibakisha Uingereza nzima katika muungano wa forodha wa Umoja wa Ulaya hadi pale mpango wa kudumu wa biashara baina ya pande hizo utakapo kamilika.

Hata hivyo, waziri mkuu, Theresa May amesema kuwa anaamini kwa akili na moyo wake kwamba uamuzi uliofikiwa katika rasimu hiyo ya makubaliano, unatilia maanani kwa maslahi ya taifa la Uingereza.

 

Spika Ndugai ampiga kijembe Msigwa 'Najua roho inamuuma sana'
Breaking News: Mbunge wa jimbo la Temeke (CUF) ajiuzulu

Comments

comments