Uingereza imetoa msaada wa shilingi Bilioni 307.5 kwa Tanzania kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika elimu, mapambano dhidi ya rushwa na uboreshaji huduma za afya.

Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Penny Mordaunt ametangaza msaada huo alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa fedha hizo zinatolewa kwa ajili ya kuunga mkono vipaumbele vya Rais Dkt. Magufuli ambapo shilingi bilioni 124.5 zitaelekezwa katika kuinua ubora wa elimu hususani kutoa fursa ya elimu kwa watoto wa kike na wenye ulemavu, shilingi Bilioni 23.5 zitaelekezwa katika kuunga mkono juhudi za kupambana na rushwa, na shilingi bilioni 160 zitaelekezwa katika kuboresha huduma za afya.

“Tunafanya hivi ili kudhihirisha dhamira yetu ya kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wetu, tunataka kujielekeza katika kuhakikisha Rais Magufuli anafanikisha ahadi zake kwa Watanzania na tunafurahi kuwa wadau muhimu wa hilo,” amesema Mordaunt.

Kwa upande wake, Rais Dkt. Magufuli amemshukuru, Penny Mordaunt kwa msaada huo na amemuomba kufikisha shukrani zake kwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May kwa mchango mkubwa ambao Uingereza hutoa kuchangia bajeti ya Serikali na kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.

 

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 11, 2018
Diwani mwingine afukuzwa Chadema