Wenyeviti wa Halmashauri na Mameya nchini wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kwenye Mamlaka za Serikali za mitaa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Pongezi za Viongozi hao zimetolewa mara baada ya kutembelea miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali katika Jiji la Dodoma, ikiwemo jengo la Ikulu ya Chamwino, ujenzi wa Mji wa Serikali ‘ Magufuli City’ na ule wa jengo la Machinga.

Akizungumza kwa Niaba ya Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo, Japhari Juma Nyaigesha amesema Rais Samia anapaswa kupongezwa na kwa kuwaletea wananchi miradi ya maendeleo.

Amemesema, wao kama viongozi wanaahidi kusimamia kwa weledi na umakini miradi inayoletwa na Serikali katika Halmashauri zao, ili wananchi iweze kuwanufaisha Wananchi.

Nyaigesha amesema Serikali imekuwa ikipeleka fedha nyingi kwenye Halmashauri kwa lengo la kuhakikisha miradi inatekelezwa na kukamilika kwa wakati hivyo ni jukumu lao kuhakikisha fedha zinazotolewa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akipeleka fedha nyingi kwenye halmashauri , hivyo ni wajibu wetu wastahiki mameya na wenyeviti wa halmashauri kuhakikisha tunasimamia kwa umakini mkubwa ili kumsaidia Rais aweze kutimiza majukumu yake ya kuwahudumia wananchi,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sera na Uratibu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Paul Sangawe amewataka viongozi hao kuwa na maono na dira kwa kutafsiri kwa vitendo ambavyo wananchi wataweza kuona na kuhakikisha wanasimamia mipango ya maendeleo kwa kutumia mapato ya ndani ili kuleta maendeleo kwa wananchi.

Aidha, ametumia nafasi hiyo kuwataka Viongozi hao kuunga mkono juhudi za Viongozi wa Kitaifa, kwa kuhakikisha wanaeleza Wananchi kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali kwenye maeneo yao.

Awali, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba iliyopo Mkoani Dodoma, Comrade Sambala Saidi amesema wao kama viongozi Wana wajibu wa kudumisha ushirikiano baina ya Mameya, wenyeviti wa Halmashauri na kada mbalimbali za kiraia.

Senzo: Mayele akiondoka Young Africans, nitaondoka
Hujaji afariki Makka, Saudi Arabia