Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), leo umetiliana saini na kampuni ya M/S China Civil Engeneering Construction Cooperation kutoka China (CCECC) mkataba wa  ujenzi wa barabara za Juu ‘Interchange’ katika makutano ya barabara ya Sam Nujoma na Mandela Ubungo jijini Dar es salaam.

Mkataba huo unamtaka Mkandarasi kampuni ya CCECC kutoka China kuanza ujenzi huo mara moja na ujenzi huo unatarajiwa kutumia takriban miezi 30 hadi kukamilika kwake.

Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS Eng. Patrick Mfugale amesema zaidi ya shilingi Bilioni 177.4 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo utakaowekewa jiwe la msingi mwezi machi mwaka huu.

“Hakikisheni mnaanza ujenzi mara moja kwani Serikali imeshakamilisha taratibu zote na tayari kiasi cha shilingi bilioni 2.1 kimelipwa kwa ajili ya fidia kwa wananchi walioguswa na mradi huo”. Amesema  Eng. Mfugale.

Aidha, ujenzi wa Ubungo interchange unajengwa kwa fedha ya mkopo kutoka Benki ya Dunia ambapo Serikali kwa upande wake imeshalipa fidia ya zaidi ya shilingi bilioni 2.1.

Vile vile, amesema kuwa zaidi ya magari 65,000 yanapita kila siku katika katika makutano ya barabara za morogoro, Mandela na sam Nujoma eneo la Ubungo hali inayosababisha msongamano katika barabara ya Morogoro ambayo ndio lango kuu la kuingia jijini Dar es salaam.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya CCECC, Jiang Yigao amemhakikishia Eng. Mfugale kuwa wataanza maandalizi ya ujenzi huo mara moja na watafanya kazi hiyo kwa wakati.

 

Mrema amshukuru Rais Magufuli kwa matibabu
Nasser Al Khelaifi: Marco Verratti Hauzwi