Ripoti ya ukaguzi wa manunuzi ya umma uliofanywa na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa mwaka wa fedha 2014/2015, imebainisha uwepo wa harufu ya rushwa kwenye taasisi za 9 za serikali zilizopitiwa na ukaguzi huo huku Timu ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikiwa miongoni mwa taasisi hizo.

Akisoma matokeo ya ukaguzi huo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dar es Salaam katika makao makuu ya PPRA, Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Balozi Matern Lumbanga ameitaja NEC kuwa kati ya taasisi 9 zilizobainika kuwa na viashiria vya rushwa kwa kiasi kikubwa na kwamba Mamlaka hiyo itayapeleka majina ya taasisi hizo katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Na Rushwa (TAKUKURU).

“Taasisi ambazo zimebainika kuwa na viashiria vya rushwa kwa asilimia zaidi ya 20 zitawasilishwa TAKUKURU kwa uchunguzi zaidi,” alisema Balozi Lumbanga.

Balozi Lumbanga alizitaja Taasisi hizo pamoja na asilimia za viashiria vya rushwa kuwa ni NEC (29%), Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (21), Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda (22%), Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo (24%), Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma (28%), Agricultural Input Trust Fund (28%), Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi (20%) na Halmashauri ya Wilaya ya Karatu (31%).

Aidha, NEC ilitajwa kuwa kati ya Taasisi 17 zilizofanya vibaya zaidi katika ukidhi wa sheria katika manunuzi ya umma. Taasisi nyingine 16 zilizotajwa pamoja na NEC ni Halmashauri ya WILAYA YA Mpanda, Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Tume ya Ajira, Kituo cha Uwekezaji Tanzania, STAMICO, Halmashauri ya wilaya ya Mbozi, Halamashauri ya Kibondo, HALMASHAURI YA Wilaya ya Kigoma, Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kampuni ya Reli Tanzania, Halmashauri ya Wilaya ya Namnyumbu, Taasisi ya Sataratani ya Ocean Road, Halmashauri ya Wilaya ya Kyela na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Lindi.

Hata hivyo, Balozi Lumbanga alieleza kuwa ukaguzi huo ulibaini kuwepo kwa ongozeko kidogo la kiwango cha uzingatiaji wa sheria kati ya taasisi nunuzi zilizokaguliwa.

“Matokeo ya ukaguzi yamebaini ongezeko kidogo la kiwango cha uzingatiaji wa sheria kutoka wastani wa asilimia 65 za mwaka jana hadi kufikia asilimia 69. Aidha, wastani huu bado uko chini ya lengo lililowekwa la asilimia 75,” alisema Balozi Lumbanga.

 

Kwanini Hukupata Ajira Ingawa Ulijibu Vizuri Maswali Ya Usaili..?
Makala: Dk. Magufuli, Dk. Slaa Wameungana Rasmi Kimkakati Kuung'oa Mbuyu