Marekani imetangaza kuyafungia makampuni 28 ya China kwa madai ya kushiriki katika zoezi linalotajwa kuwa la ubaguzi na ukandamizaji wa kidini dhidi ya watu wa kabila la Uighurs wa jimbo la Xinjiang.

Kwa mujibu wa taarifa za Kituo cha Haki za Binadamu, zaidi ya watu milioni moja wa kabila la Uighurs hususan waumini wa dini ya Kiislam wanashikiliwa katika vituo maalum nchini China na imetangazwa marufuku ya kuvaa mavazi ya kufunika sura (mask).

Taasisi hizo zimeingia kwenye orodha maalum ambayo haitaziruhusu kununua au kuuza bidhaa kwa makampuni ya Marekani bila kupata kibali maalum kutoka Ikulu.

Taasisi hizo za China zilizoathiriwa na hatua hiyo ya Marekani ni pamoja na taasisi za umma na makampuni ya teknolojia yanayojihusisha na masuala ulinzi wa kutumia viangalizi kama kamera.

China iko katika ukosoaji mkubwa kufuatia hatua yake ya kuwakusanya wananchi hasa wa kabila la Uighurs ambao wengi wao ni waislamu na kuwaweka katika vituo maalum ambavyo wanaviita ‘vyuo vya ufundi stadi’ vyenye lengo la kuwaondoa katika mawazo ya kigaidi na misimamo mikali ili wawe raia wema.

Hata hivyo, hatua hiyo imekosolewa vikali kwani inaonekana kuwa wanachofanyiwa watu hao ni kuwekwa kwa nguvu katika vituo hivyo. Hatua hiyo inatajwa kuwa ni kama kuwaweka gerezani kwani hawana uhuru wa kuziona familia zao hadi pale Serikali itakapoamua kuwaachia tena.

Shirika la labari cha Uingereza (BBC), iliruhusiwa kufanya makala ndani ya vituo hivyo chini ya uangalizi wa maafisa wa Serikali ya China. Baadhi ya video zinawaonesha watu hao wakifundishwa lugha ya Kichina na falsafa ya kupenda chama pekee cha siasa cha nchi hiyo. Pia, inawaonesha wakifundishwa kucheza nyimbo mbalimbali za utamaduni wa Kichina.

Hata hivyo, ndani ya vyumba wanavyolala watu hao wanaishi kama bwenini wakichangia choo ndani ya vyumba, hali inayowafanya wakosoaji wa China kusisitiza kuwa sehemu hiyo sio chuo cha mafunzo bali ni gereza.

Maafisa wa Serikali ya China wamekanusha vikali taarifa kuwa sehemu hizo ni magereza wakidai kuwa hakuna magereza inayowafundisha watu kuchora, kucheza na kuwaweka darasani kusoma stadi za kazi na maisha.

“Umewahi kuona wapi duniani kuna gereza kama hili? Afisa wa Serikali aliyehojiwa na BBC alieleza. Hapa watu wanafanya kile wanachopenda ili wawe watu bora zaidi huko nje. Walikuwa na mawazo ya kigaidi, sasa wanatayarishwa kuwa watu wema zaidi,”alisema.

Kituo hicho cha habari kimeeleza kuwa wakati kinarekodi sehemu za vyumba vya eneo hilo kiliona ujumbe ulioandikwa kwa mkono, “moyo wangu naomba usivunjike.” Maandishi ambayo yanaonesha kuna hali ambayo inawaumiza watu wanaowekwa kwenye kituo hicho sio ridhaa yao.

Mmoja kati ya wananchi wa Uighurs aliyechaguliwa na maafisa wa Serikali kuhojiwa na BBC ndani ya jengo hilo alieleza kuwa aliamua mwenyewe na kwamba alikuwa ana mawazo ya kufanya ugaidi na sasa anapata mtazamo mwingine bora wa maisha.

Taasisi zilizofungiwa na Marekani zinadaiwa kusaidia katika kudukua taarifa za watu wa kabila la Uighurs na kuisaidia Serikali ya China kufanikisha kinachoendelea.

Hii sio mara ya kwanza Marekani kuzifungia kampuni za China. Mei mwaka huu, Rais Donald Trump alitangaza kuyafungia makampuni yote yaliyo chini ya Kampuni kubwa ya Huawei kwa madai ya kuhusika kuingilia masuala ya kiusalama ya nchi hiyo.

Mohamed Salah kuwakabili Man Utd Oktoba 20
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Oktoba 8, 2019