Ngome ya Ukawa inayoundwa na vyama vinne vya upinzani vya NCCR-Mageuzi, NLP, CUF na Chadema vimetofautiana na Jeshi la Polisi nchini lililopiga marufuku mikutano na maandamano ya kisiasa nchi nzima hadi pale litakapotangaza tena.

Tangazo hilo rasmi la Jeshi la Polisi lilitolewa hivi karibuni na msemaji wa Jeshi hilo, Advero Senso lilieleza kuwa wameamua kupiga marufuku mikutano yote ya kisiasa kwa kuwa taarifa za uhakika za kiusalama zimeeleza kuwa bado kuna mihemko ya kisiasa ambayo inaweza kuhatarisha amani iwapo mikutano hiyo itaruhusiwa.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema ambaye ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe ameeleza kuwa mikutano yao iko palepale kwa kuwa waliomba kibali polisi na walipewa na kwamba bado hawajapokea barua rasmi ya kuzuia mikutano hiyo.

“Mkutano wetu bado uko pale pale, hakuna kilichobadilika msipende kusikiliza taarifa za kwenye mitandao. Hadi sasa hatujapewa barua kutuzuia, kibali tunacho na taarifa nyingine kuhusiana na mkutano huo nitatoa kesho asubuhi (leo),” Mbowe alimwambia mwandishi wa gazeti la Nipashe.

Ukawa walikuwa wamepanga kufanya mikutano yao leo nchi nzima ambapo kwa Dar es Salaam ulipangwa kufanyika katika viwanja vya Jangwani na kuhudhuriwa na viongozi wa Ukawa pamoja na mgombea wake wa urais, Edward Lowassa.

Sababu Za Mama Regina Lowassa Kuikataa Ofa Ya Chadema Hizi Hapa
Kasi Ya Rais Magufuli Yaanza Kuwanyoosha Hawa