Wakati Tume ya Uchaguzi ikiendelea na zoezi la kutangaza matokeo ya Urais, vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa vimetangaza kutokubaliana na mwenendo wa utangazaji wa matokeo hayo ikiwa ni pamoja na kutofautiana kwa matokeo yanayotangazwa na yale yaliyosainiwa vituoni.

Wakiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, wenyeviti wenza wa Ukawa, Freeman Mbowe (Chadema) na James Mbatia (NCCR-Mageuzi) pamoja na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema, Profesa Abdallah Safari wamedai kuwa pamoja na kutofautiana kwa kura zinazotangazwa, NEC wameshirikiana na CCM pamoja na Jeshi la Polisi kuwahujumu ili kukipendelea chama tawala.

“Yapo mambo mengi yanayotendeka dhidi ya Umoja wetu wa Ukawa, na kipekee mgombea wetu wa urais, mheshimiwa Edward Lowassa katika kuhakikisha hapati nafasi ya kushinda kiti cha urais, sambamba na kujaribu kupunguza kwa nguvu isipokuwa halali idadi ya wabunge wetu katika Umoja wetu wa Ukawa, kwa kutumia Jeshi la Polisi na kutumia taratibu ambazo ni za siri ndani ya Tume ya Uchaguzi,” alisema Freeman Mbowe.

Aidha, viongozi hao wa Ukawa walieleza kuwa vijana wao waliokuwa wakifanya kazi ya kukusanya matokeo katika vituo mbalimbali kwa njia ya kielektoniki, walikamatwa kinyume cha sheria katika eneo la Mwananyamala na mifumo ya kuhesabiwa iliharibiwa na jeshi la polisi.

Waliwataka Jeshi la polisi kuwaachia vijana hao ambao miongoni mwao wamo wataalam wa TEHAMA kutoka Kenya na Korea. Wamedai kuwa kazi waliyokuwa wakiifanya vijana hao ni sawa na kazi ya kujumuisha matokeo iliyokuwa ikifanywa na CCM katika eneo la Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Vijana hao nane walikamatwa na kufikishwa mahakamani na wanashitakiwa kwa makosa ya kusambaza taarifa za uongo kuhusu matokeo ya urais majimboni kupitia akaunti za Chadema, kufanya kazi nchini bila kibali.

Vijana hao wamenyimwa dhamana kwa ombi maalum la Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali.

Matokeo Urais Zanzibar ‘Vutankuvute’, Maalim Seif Anyemelewa
Wabunge Waliotangazwa Jioni Hii