Ukusanyaji ushuru wa maegesho ya magari katika Jiji la Arusha imeingia utata baada ya kugonganisha mtaani watumishi wa Jiji na wale wa kampuni ya J.N. Mining iliyokuwa imepewa kazi ya kukusanya ushuru.

Kufuatia hali hiyo askari wa Jiji la Arusha kwa amri waliyopewa na uongozi wa jiji waliwakamata wafanyakazi wa J.N. Mining kwa madai kuwa zabuni yao ya kufanya kazi hiyo ilimalizika Juni 30, mwaka huu.

Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro alisema kitendo cha wafanyakazi wa J.N. Mining kuingia barabara tena kufanya kazi hiyo ni ukiukwaji wa taratibu za zabuni hiyo, kwani muda wao ulimalizika Juni 30, mwaka huu.

Alisema Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Justin Nyari aliombwa kuongeza mwezi mmoja wa kukusanya ushuru wakati jiji likijipanga, lakini alikataa, hivyo kuamua wafanyakazi wa Jiji waifanye kazi hiyo kwa muda kuanzia Julai Mosi.

“Hii kazi ni ngumu sana, Jiji hatuwezi kuifanya kwa sasa tunatumia risiti za vitabu kwa muda wa siku 14 tu na baadaye tutaitangaza ili wazabuni wapatikane na kuifanya kazi hii,” alisema.

 

Mkurugenzi huyo wa J.N. Mining alimtaka Meya Lazaro kuwaachia wataalamu kufanya kazi yao kitaalamu na kuacha kuingiza siasa katika mambo ya msingi yenye kuliongezea jiji mapato.

Pia amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kukaa na timu yake na kuangalia namna ya kufanya ili jiji lisikose mapato kwa kuingiza siasa katika kazi hiyo.

Mitihani Miwili Ya Serengeti Boys Hii Hapa
Muswada wa Sheria ya Ndoa Kufika Bungeni Mwaka Huu