Siku moja baada ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza kuahirisha kufanya maandamano na mikutano nchi nzima kupitia oparesheni walioipa jina la UKUTA ( Septemba Mosi) na kisha kuitaja Oktoba Mosi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameitaja siku hiyo kuwa siku maalum ya kupanda miti itakayohusisha majeshi yote.

Serikali ilitangaza Septemba 1 kuwa siku maalum ya kuadhimisha miaka 52 ya JWTZ ambapo ilitumia siku hiyo kama siku ya jeshi hilo kuungana na wananchi kufanya usafi mitaani nchi nzima, siku ambayo Chadema walikuwa wamepanga kufanya maandamano.

Akizungumza jana baada ya kushiriki usafi na JWTZ katika maeneo mbalimbali mkoani Dar es Salaam, Makonda amesema Oktoba Mosi itakuwa siku maalum kwa ajili ya upandaji miti katika jitihada za kuboresha mazingira ambapo majeshi yote nchini yatashiriki.

Aidha, makonda alimepiga marufuku kufanyika kwa mikutano au maandamano yoyote isipokuwa mikutano itakayokuwa inajadili shughuli za maendeleo.

“Watakaopewa kibali cha kufanya mikutano ni wale watakaokuwa wanajadili maendeleo, lakini si wapiga kelele,” alisema Makonda.

Makonda amesema kuwa jumla ya miti milioni 4 inatarajiwa kupandwa siku hiyo ambayo kamati yote ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Dar es Salaam itaungana na majeshi yote pamoja na wananchi katika kupanda miti hiyo.

CUF yampisha Magufuli kufanya Mkutano Pemba
Video: Makonda ashiriki usafi na JWTZ, Atangaza Oktoba 1 siku ya kupanda miti