Ujerumani, Hispania, Ufaransa na Uingereza zimemuamkia upya Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro zikimtaka achague moja kati ya kuitisha uchaguzi ndani ya siku nane au la wamtambue mpizani wake kama Rais wa mpito.

Rais Maduro anashinikizwa na nchi hizo ikiwa ni siku chache tangu Marekani iseme kuwa inaunga mkono uamuzi wa mpinzani wake, Juan Guaido kujiapisha kuwa Rais wa kipindi cha mpito, Jumatano wiki hii wakati maelfu ya waandamanaji wakiwa mitaani.

Maduro aliishutumu Marekani kwa kitendo hicho akidai kuwa ni kutaka kupokonya madaraka halali na kuchochea machafuko.

Wakati nchi hizo zikimpa onyo hilo Maduro, Urusi, China, Mexico, Cuba, Uturuki, Bolivia na washirika wao wamekosoa vikali tamko la Marekani na kueleza kuwa wao wanamuunga mkono na wanamtambua Maduro kama Rais halali wa nchi hiyo.

Katika tamko lake, Urusi imeeleza kuwa tamko la Marekani linachochea umwagaji damu nchini humo.

“Tunachukulia hatua ya kutaka kupokonya madaraka ya Serikali halali nchini Marekani kama hatua ya kutaka kuleta umwagaji damu na kuvunja sheria za kimataifa,” Reuters inaikariri taarifa ya Ikulu ya Urusi. “Tunamtambua Maduro kama kiongozi halali wa Serikali,” iliongeza.

Rais Maduro aliapishwa mwezi uliopita ili aingoze nchi hiyo kwa kipindi cha pili, baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa mwezi Mei mwaka jana ambao unalalamikiwa na mpinzani wake kuwa uligubikwa na wizi wa kura, hivyo wamedai matokeo hayatambuliki na wanataka uchaguzi urudiwe.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Januari 27, 2019
300 wahofiwa kufa baada ya bwawa la maji kubomoka Brazil

Comments

comments