Maria na Consolata ni wasichana waliozaliwa wakiwa wameungana na sasa wamekuwa na furaha kubwa baada ya kufanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho ya kidato cha sita.

Mapacha hao wenye umri wa miaka 19 walikuwa wanasoma katika shule ya Sekondari ya Udzungwa mjini Iringa nchini Tanzania, wamefaulu kwa kupata daraja la pili katika masomo yao ya kidato cha sita na kuwa na matumaini kuwa ndoto yao ya kuwa walimu hapo baadaye inaelekea kutimia.

“Tulipokea matokeo yetu tukiwa kwenye mazingira ya nyumbani tu, tukiendelea na shughuli zetu za kila siku, tukaambiwa matokeo yametoka na tumefanya vizuri, tulikuwa tukiwaza kabla ya hapo, unajua kwenye mitihani ya mwisho huwezi kujiamini sana,” amesema Consolata.

Baada ya matokeo hayo, Maria na Consolata wamesema kuwa wanapendakuendelea na masomo yao ya elimu ya juu katika chuo kilichopo katika mkoa wanaoishi tofauti na vyuo vingine au kama ilivyo kwa wanafunzi wengine ambao wangependa kubadili mazingira, hivyo wamechagua Chuo Kikuu Cha Ruaha.

“Kwanza tunapenda mazingira ya Iringa, hatukutaka kwenda Dar es Salaam kwa sababu ya kwanza tunapenda kuishi pamoja na walezi wetu Masista waliokuwa wanatulea tukiwa wadogo na pili mikoa mingine ni mbali na tunapoishi,” alisema.

Kadhalika, mapacha hao wamesema wamechagua kubakia mkoani kwao kwa sababu ya hali yao, wamesema hawatamudu kuishi kwenye mazingira ya joto. “Mji wa Iringa ni baridi, hali hii tumeizoea.”

Aidha, wametoa wito kwa wazazi, wamesema hakuna linaloshindikana iwapo wazazi watawajibika ipasavyo kwa watoto wao wenye ulemavu, wawaone kama watoto wengine na kuwapa mahitaji yao ya msingi, wawawezeshe, wawapatie nafasi ya kujiendeleza maana wakiwezeshwa wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri.

” Wazazi washukuru Mungu kupata watoto wenye changamoto kama wao wasione kuwa na mtoto mlemavu ni laana.”

Video: Ndege ya Serikali kusafirisha mwili wa mke wa Dkt. Mwakyembe
Video: Msechu aachia mpya 'Yakawa'