Mwishoni mwa wiki kulikuwa na tukio la kipekee lililopelekea kutokea kwa maamuzi ya kipekee na kuweka rekodi ya kipekee kwenye siasa za Tanzania.

‘Upekee’ huo ulianzia Bungeni na kukamilishwa zawadi ya bakora nzito ya Mkuu wa Nchi ambaye hivi sasa wananchi wamempa jina la ‘Mzee wa Kuwanyoosha’ ingawa yeye alijipa kazi anayoitekeleza kwa dhati bila upendeleo ya ‘kutumbua majipu’.

Tunaweza kusema ni upekee kwani hakuna aliyewahi kufikiria kama Kiongozi wa ngazi ya Juu kama Waziri anaweza kuamua kula mvinyo wakati anafahamu kabisa kuwa anaingia katika Bunge tukufu kujibu maswali mazito yanayolenga mstakabali wa Taifa.

Ni maajabu ya ‘Kitwanga’ kwa mtu aliyetakiwa kuwa mstari wa mbele kuagiza jeshi la Polisi kuwakamata Bodaboda wanaokunywa viroba wakati wako kazini wakibeba roho za watu, madereva wa mabasi wanaokunywa mvinyo kabla ya kuanza safari inayobeba roho za watu, walimu wanaotoka kushtua mvinyo kabla ya kuingia darasani na watumishi wengine wa umma wanaoendekeza ulevi kazini. Lakini yeye ndiye anayevuta mvinyo na kutupia suti kabla ya kuanza kujibu maswali mazito na muhimu yanayoekezwa kwa wizara yake iliyoshikilia roho ya usalama wa ndani wa nchi.

Baada ya kukuchorea picha hiyo, ni vyema nikakukumbusha tukio ambalo kila mmoja sasa analifahamu kutokana na upekee wake na maajabu yake. Jana, Rais John Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga baada ya kuingia Bungeni akiwa amelewa na kujibu maswali ya wizara yake.

Hata hivyo, uamuzi huo wa Rais John Magufuli ambao ni wa kipekee na unaoonesha kuwa mzee wa Kuwanyoosha ananyoosha bila kujali anayetakiwa kunyooshwa ni nani, unaweza kuwa umepokelewa kwa sura mbili na Kambi ya Ukawa ambayo hivi karibuni ilikuwa imeanzisha kampeni maalum iliyolenga kuhakikisha Kitwanga anajiuzulu au Rais anamng’oa.

Katika upande wa kwanza, Ukawa wanaweza kuwa wamefurahia sana uamuzi wa Rais Magufuli kumtimua Kitwanga kwakuwa ndilo lililokuwa lengo lao japo sio kwa sababu hiyo. Lakini upande wa pili wanaweza kuwa wamepoteza pointi 3 muhimu sana kwani ni dhahiri kuwa lengo lao lilibeba mkakati mzito ambao sasa wanaweza kulazimika kuutua au kupunguza nguvu.

Na huenda ‘Ulevi’ wa kitwanga ukawa sababu kubwa ya kuwaharibia mkakati wao ambao kama ungefanikiwa kwa kumuona anajiuzulu au anaondolewa na Rais ungekuwa ushindi mkubwa kwao.

Hii ni kwa sababu kampeni waliyoianzisha Ukawa Bungeni ililenga kumuondoa Kitwanga katika nafasi ya Uwaziri akiwajibika kwa sakata la mkataba tata kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi.

Akisoma hotuba mbadala Bungeni, Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema (Chadema), alimtaka Kitwanga kujitathmini na kuchukua hatua ya kujiuzulu kwani Kampuni ya INFOSYS ambayo yeye pia ni mbia ilihusika moja kwa moja katika utekelezaji wa mkataba huo na ililipwa mamilioni ya fedha.

“Kwa vile Waziri wa Mambo ya Ndani anahusika kwa karibu katika Mkataba huu kupitia Kampuni yake ya INFOSYS na vile vile Jeshi la Polisi liko chini yake, je? haoni kuwa ni busara kwa yeye kujiuzulu ili kutoa nafasi ya Uchunguzi kuepusha mgongano wa maslahi ndani ya Jeshi la Polisi na kwenye Kampuni ambayo yeye ni mmoja wa wamiliki,” Lema alisema.

“Kampuni ya INFOSYS (inayomilikiwa na Mhe. Kitwanga) imedai kulipwa na Jeshi la Polisi, takribani Dolla za Marekani 74,000,” Lema alieleza katika sehemu nyingine ya hotuba yake ambayo hata hivyo ilikutana na vizuizi vingi vya kanuni za Bunge kutokana na kuwa na baadhi ya maneno yasiyokubalika kikanuni.

Katika hatua nyingine, Lema ambaye aliweka wazi kuwa kabla hajaandika hotuba yake alikaa na Kitwanga nyumbani kwake na kula ugali pamoja, alimuonya kuwa suala la mkataba wa Lugumi litamgharimu kwani linalipaka tope Jeshi la Polisi na kwamba wabunge watamgeuka na kumuondoa, anaweza kuwa alianza kuuona mwisho wake katika nafasi hiyo kwa namna yoyote.

Endapo Ulevi usingemponza Kitwanga, ni dhahiri kuwa Ukawa wangeendelea kushinikiza ajiuzulu kwa sakata la Mkataba wa Lugumi. Huenda wakaulaumu ulevi wake kuwaharibia sehemu ya kampenii yao ambayo bila shaka walikuwa wamejipanga kimkakati. Hata hivyo, bado wanaweza kuendelea na kampeni hiyo kwani wanaotuhumiwa ni wengi.

Hapana shaka kuwa kama angekutwa na hatia na kugoma kujiuzulu, Rais Magufuli angemuondoa maramoja. Hii imedhihirika baada ya kumuondoa kwa kosa la kukiuka miiko ya utumishi wa umma kwa kulewa kazini.

Kama alivyosema Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, Rais Magufuli ameonesha kuwa ‘hataki mchezo’.

Mashindano ya ‘Big Brother Africa’ yatupwa kapuni
2015/16 Tunaikamilisha Kwa ‘Kuiua’ Ndanda FC

Comments

comments