Chama cha soka Korea Kusini kimemtimua kocha Uli Stielike baada ya kupoteza mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia kwa kufugwa na Qatar mabao 3-2 siku mbili zilizopita.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 62, alisaini mkataba wa miaka minne wa kukinoa kikosi cha Korea Kusini (Taegeuk Warriors), na jukumu kubwa alilokua amepewa ni kuhakikisha anaifikisha timu ya taifa ya nchi hiyo kwenye fainali za kombe la dunia za 2018 zitakazochezwa nchini Urusi.

Stielike raia wa Ujerumani, alionekana mwenye huzuni baada ya kikosi chake kupoteza mchezo huo mjini Doha, hali ambayo iliifanya Korea kusini kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi A kwa tofauti ya point moja, wakifuatiwa na Uzbekistan huku wakiongozwa na Iran.

Tayari Iran imeshafuzu kucheza fainali za kombe la dunia za 2018 kwa kuongoza msimamo wa kundi hilo, baada ya kufikisha Point 20 ambazo haziwezi kufikiwa na yoyote.

Hofu imetanda kuhusu mustakabali wa kufuzu kwa Korea Kusini, kufuatia michezo miwili iliyosalia kutazamwa kama mtihani mkubwa kwa timu hiyo ya mashariki ya mbali.

Korea Kusini watacheza dhidi ya Iran mwishoni mwa Agusti na kisha watamalizia michezo ya kundi hilo kwa kupambana na Uzbekistan ugenini mwanzoni mwa mwezi Septemba, na kama watashindwa, watafifisha matumaini ya kufuzu.

Korea Kusini imeshashiriki fainali za kombe la dunia mara nane, na mafanikio makubwa waliyoyapata, ni kucheza hatua ya nusu fainali mwaka 2002, walipokua wenyeji.

Godzilla amvaa Nikki Mbishi, ‘nitamrudisha...'
Kasesela akesha mgodini kuokoa mwili wa mchimbaji