Mshambuliaji wa Tanzania Thomas Ulimwengu ameachana na soka la Ulaya baada ya kumalizana na klabu ya AFC Eskilstuna ya Sweden aliyokuwa akiitumikia na kujiunga na timu ya El Hilal ya Sudan.

Mchezaji huyo tayari amekamilisha usajili wa kujiunga na timu ya El Hilal kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Wakala wa mchezaji huyo, Jamal Kisongo ametaja sababu kubwa ya kumrejesha Ulimwengu barani Afrika ni kutokana na kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu na kukosa kibali cha kazi nchini Sweden.

”Tukumbuke amekaa miaka miwili hajatumikia na alikuwa na tatizo la kibali cha kazi kwahiyo ili arudi kwenye kiwango chake ilibidi arudi kwenye timu bora barani Afrika, lengo ni kurejea kwenye kiwango kizuri na baada ya muda atarudi Ulaya” amesema Kisongo.

Hata hivyo Ulimwengu anarejea uwanjani baada ya kupona maumivu ya goti kufuatia kufanyiwa upasuaji katika hospitali ya Taasisi ya Sayansi ya Michezo mjini Cape Town, Afrika Kusini mwaka jana na kupitia kipindi kirefu cha mazoezi ya kujiweka fiti.

Ulimwengu alihamia Ulaya baada ya kushinda mataji makubwa akiwa na  Mazembe kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Super Cup ya Afrika na pamoja na kucheza Klabu Bingwa ya Dunia.

Aidha Al Hilal ni moja kati ya timu zinazoshiriki michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika katika hatua ya makundi.

 

 

Urusi 2018: Nani atabeba Kombe? Tuimulike Australia
Babu Tale arudi uraiani