Ulinzi umeimarishwa katika barabara zote zinazoingia katika makao makuu ya jeshi la polisi, Ohio jijini Dar es Salaam, wakati jeshi hilo likisubiri ujio wa waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwa ajili ya kumhoji.

Lowassa anatarajiwa kuhojiwa na ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) ingawa sababu za kuhojiwa kwake bado hazijawekwa wazi.

Askari wenye silaha wametanda katika barabara zote zinazoingia katika eneo hilo ingawa wananchi wanaruhusiwa kupita na kuendelea na shughuli zao za kawaida.

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amesema kuwa ataitikia wito huo lakini anahisi umetokana na kauli yake aliyoitoa hivi karibuni wakati wa futari iliyoandaliwa na madiwani wa chama hicho jijini Dar es Salaam kuhusu kuachiwa kwa viongozi wa Jumuiya ya Uamsho.

Lowassa alisema kuwa alitoa kauli hiyo kuhusu mashekhe hao wanaoshikiliwa gerezani kwa uchochezi tangu mwaka 2012 kwakuwa ilikuwa ni sehemu ya ahadi zake kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

“”Nilisema hivyo kwa sababu kuna Sheikh wakati wa kunikaribisha alisema japo tunasherekea Eid el Fitr bado kuna masheik wenzetu wanateseka. Nilisema hivyo kwa sababu nilishaahidi kwenye kampeni zangu kwamba tukishinda tutawatoa hao masheikh,” alisema Lowassa.

DCI Robert Boaz aliwaeleza waandishi wa habari kuwa msemaji wa jeshi la polisi, Advera Bulimba ndiye anayeweza kulizungumzia lakini msemaji huyo alirudisha mpira kwa Lowassa mwenyewe kuwa msemaji wa suala hilo.

Kichanga chatimba bungeni, Mamaye aistaajabisha dunia
Mwinyi ampa tano Magufuli