Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na Watu Wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga amewaagiza waajiri nchini kuhakikisha wanawaruhusu wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi wanavyoviridhia.

Nderiananga ametoa kauli hiyo leo Juni 05, 2021 mkoani Morogoro wakati akifungua semina ya wajumbe wa Baraza Kuu la Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO).

Amesema serikali itachukua hatua stahiki dhidi ya waajiri wanaowazuia wafanyakazi wao kujiunga na vyama vya wafanyakazi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TUICO Taifa, Paul Sangeze amesema kuna waajiri ambao hawatoi ushirikiano maeneo ya kazi hali inayochangia kukuza migogoro baina ya wafanyakazi na waajiri na hivyo kupunguza tija sehemu za kazi.

Aidha, ameiomba serikali kuhakikisha inatembelea maeneo ya kazi hasa yenye matatizo mengi ili kukuza tija, haki, heshima na maslahi ya wafanyakazi mahala pa kazi.

Wadau washauri mfumo wa mazingira uboreshwe
Hizi ndizo kesi 10 za unyanyasaji Tanzania, ubakaji watikisa