Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeipongeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kwa kuchukua hatua za haraka za kudhibiti ugonjwa wa Ebola usiingie nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya. Ummy Mwalimu jijini Dar es salaam katika hotuba yake kwa wananchi walioshiriki Matembezi ya hiyari ya kuelimisha na kuhamasisha Jamii kuzuia ugonjwa huo usiingie nchini.

Ummy Mwalimu amesema TAA inafanya jambo jema kwa kuhakikisha wasafiri wote wanaoingia nchini kupitia viwanja vya ndege wanafanyiwa ukaguzi na kutoa taarifa za afya zao kwa wale ambao watabainika kuwa na joto la mwili lisilokuwa la kawaida.

“Nawapongeza sana tena sana Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania kwa kuhakikisha nchi inakuwa salama bila kupata maambukizi ya ugonjwa huu wa Ebola, imeripotiwa sasa huu ugonjwa upo Kivu Kaskazini nchini Congo jirani na Tanzania, ambapo ni karibu na nchini na Wavuvi wanakuwa na muingiliano kwa kutoka huko na kuja nchini,” amesema Ummy Mwalimu.

Aidha, amesema pamoja na ugonjwa huo kutoingia nchini, lakini kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), tayari imeripotiwa wananchi 111 wa Kongo wamepata maambukizi na kati yao 75 sawa na asilimia 67 wamefariki, hivyo inakisiwa endapo Tanzania ikiwa na wagonjwa 100 inaweza kusababisha vifo vya watu 50.

Hata hivyo, Ummy Mwalimu amewaomba Viongozi wa Dini kutumia majukwaa yao katika mahubiri yao kutoa tahadhari kwa wananchi kuhusiana na ugonjwa huo wa Ebola, ambapo pia amewaomba wasanii wa muziki na viongozi wa Siasa nchini kutumia majukwaa yao ili kufikisha taarifa kwa wananchi juu ya ugonjwa huu.

LIVE: Mazishi ya Watanzania waliofariki dunia katika ajali ya MV Nyerere
Video: Maalim Seif aanza safari Chadema, Mhandisi aokolewa saa 48 majini