Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Tanga na Waziri wa Afya, mhe Ummy Mwalimu jana ametembelea kambi ya Timu ya Coastal Union iliyopo Eneo la Saruji jijini Tanga, ambayo hivi sasa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza na ipo nafasi ya 3 kundi B.

Mhe Ummy amewataka wachezaji wa Coastal kuongeza jitihada na kujituma ili kushinda mechi nne zilizobaki kwa lengo la kujihakikishia nafasi ya kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2018/19. “Coastal ikipanda daraja na kucheza Premier League sio tu itawezesha vijana kupata kipato bali pia itachochea uchumi na maendeleo ya Jiji la Tanga”, alisema mhe Ummy.

Katika kuhamasisha huko, mhe Ummy amekabidhi shilingi milioni 3 na nusu kwa ajili ya mishahara ya wachezaji ya mwezi Desemba na gharama za chakula.

Aidha Mhe Ummy ameahidi kuwa atatoa zawadi ya shilingi milioni 2 kwa kila mechi watakayoshinda kati ya mechi 4 zilizobaki.

Wakizungumza wakati wa tukio hilo, Kocha Mkuu wa Coastal Union Juma Mgunda amemuhakikishia mhe Ummy kuwa vijana wapo tayari kwa ushindi na hivyo anaamini hawatamuangusha. Pia, wamemshukuru Mhe Ummy kwa kujitoa kwake ili kuhakikisha Timu ya Coastal Union inapanda daraja. Tukio hilo limehudhuriwa na Mwenyekiti ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga, Said Sudi na Ndugu Salim Bawazir Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Coastal.

Mbowe, Lowassa wamtembelea Kingunge Muhimbili
Chama kuzikwa kesho Jumanne, Young Africans waomboleza

Comments

comments